Donald Trump alimhadaa Kim Jong-Un kuhusu kitufe cha nyuklia?

Generic button Haki miliki ya picha Thinkstock

Rais wa Marekani Donald Trump alimtahadharisha Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong-un kwamba ana kibonyezo au kitufe cha nyuklia kikubwa kuliko chake kwenye meza yake.

Trump alisema hayo kwenye ujumbe kupitia Twitter. Lakini je, ni kweli?

Kulipua silaha za nyuklia ni shughuli yenye utaratibu mwingi, si rahisi vile kama tuseme kubadilisha vituo kwenye runinga.

Jambo la kushangaza ni kwamba nchini Marekani msamiati wake unahusisha biskuti na mpira wa kandanda.

Ingawa tamko la kuwepo "kitufe cha nyuklia" linafahamika sana, ukweli ni kwamba ni ufupisho wa shughuli ndefu.

Kwa hivyo, jibu liko wazi.

Katika uhalisia, Donald Trump hata kitufe chochote cha kufyatua au kurusha silaha za nyuklia.

Trump ana nini?

Mnamo 20 Januari mwaka jana, msaidizi wa rais wa kijeshi aliyekuwa amebeba mkoba wa ngozi alihudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Donald Trump alifika akiandamana na Rais Obama.

Baada ya Trump kuapishwa, msaidizi huyo - na mkoba wake - alihama na kwenda kwa Trump.

Mkoba huo hufahamika kama "mpira wa kandanda wa nyuklia".

Mkoba huo unahitajika kutoa idhini ya kurushwa kwa silaha za nyuklia za Marekani na - kwa nadharia - huwa hauondoki karibu na rais wa Marekani.

Agosti, mtaalamu mmoja aliambia CNN kwamba hata Trump anapokuwa anacheza gofu, mkoba huo huwa anaubeba kwenye kigari cha kusafirisha wachezaji uwanjani.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Shirika la habari la taifa la Korea Kaskazini lilitoa picha ambayo ilidaiwa kuwa ya kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong-un akisimamia bomu la haidrojeni mwishoni mwa mwaka jana

Mkoba huu una nini?

Ukapewa nafasi ya kuchungulia kuangalia nini huwa ndani ya mkoba huo ambao hufahamika kama mpira wa kandanda wa nyuklia, unaweza kusikitika.

Hamna kitufe chochote cha silaha za nyuklia.

Na pia hakuna saa yoyote, inayoashiria mwisho wa dunia au vita vya Armageddon.

Kenya kuzalisha kawi ya nyuklia kufikia 2027

Badala yake, ndani mna vifaa vya mawasiliano na vitabu ambavyo vina mipango ya kivita na kijeshi iliyotayarishwa mapema.

Mipango hiyo ni ya kurahisisha kufanya uamuzi haraka.

Mwaka 1980, Bill Gulley - mkurugenzi wa zamani wa afisi ya kijeshi ikulu ya White House - alisema njia mbalimbali za kujibu mashambulio zinafaa kuwa "adimu, za wastani, au zilizotekelezwa kwa ufasaha wa hali ya juu".

Biskuti nayo ni nini?

"Biskuti" ni kadi ambayo ina mseto wa tarakimu na herufi maalum (fumbo), ambayo inafaa kubebwa kila wakati na rais.

Huwa kando na mkoba unaofahamika kama mpira wa kandanda wa nyuklia tuliouzungumzia hapa juu.

Iwapo rais atataka kuidhinisha shambulio, atatumia mkusanyiko huyo maalum wa tarakimu na herufi kujitambulisha kwa jeshi.

Baada ya kuingia madarakani, ABC News walimwuliza Trump alihisi vipi alipokabidhiwa "biskuti".

"Wanapokufafanulia maana yake, na kiwango cha maafa na uharibifu ambacho inaweza kusababisha, ni jambo ambalo linakuzindua," alisema.

"Ni jambo linalokutia wasiwasi sana, wasiwasi sana, kwa kiasi fulani."

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Trump alisema kitufe chake cha nyuklia ni kikubwa kuliko cha Kim

Msaizidi wa zamani wa kijeshi wa Bill Clinton, Robert "Buzz" Patterson, alidai wakati mmoja Bw Clinton alipoteza mseto huo wa tarakimu na herufi alipokuwa rais.

Bw Patterson alisema Clinton alizoea kuiweka biskuti hiyo kwenye mfuko wake wa suruali, ikiwa pamoja na kadi zake za benki akiwa amezifunga kwa utepe.

Asubuhi ambayo sakata ya Lewinsky iligonga vichwa vya habari, Clinton alikiri kwamba hakuwa ameiona kadi hiyo kwa muda, kwa mujibu wa Patterson.

Afisa mwingine wa ngazi ya juu - Jenerali Hugh Shelton - alidai pia kwamba Clinton aliipoteza biskuti hiyo "kwa miezi kadha".

Rais huidhinishaje shambulio la nyuklia?

Ni rais pekee ambaye anaweza kuidhinisha shambulio la nyuklia.

Baada ya kujitambulisha, atatuma amri yake kwa mwenyekiti wa jopo la Wakuu wa Majeshi.

Mwenyekiti huyo ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi wa kijeshi.

Amri hiyo itatumwa kwa makao makuu ya majeshi maalum ya Marekani katika kambi ya jeshi la wanahewa ya Offutt, Nebraska.

Maafisa wa kambi hiyo nao watawasilisha amri hiyo kwa makundi mengine ya wanajeshi kwingineko, ambao wanaweza kuwa ardhini, angani, juu ya bahari au chini ya bahari.

Amri ya kufyatua silaha hiyo husafirishwa kwa mafumbo - ambayo ni mafumo yanayofaa kuoana na mafumbo ambayo yamehifadhiwa kwenye sefu za wanajeshi walio na silaha hizo.

Amri ya rais inaweza kupuuzwa?

Rais wa Marekani ndiye amiri jeshi mkuu wa majeshi ya Marekani.

Kwa kifupi, anachokiamrisha, lazima kitekelezwe.

Lakini - pengine - kuna njia fulani hili linaweza kuzuiwa.

Novemba, kwa mara ya kwanza katika miaka 40, Bunge la Congress lilichunguza tena mamlaka ya rais kuidhinisha shambulio la nyuklia.

Mmoja wa wataalamu waliohusishwa alikuwa C Robert Kehler, kamanda wa kikosi maalum cha jeshi la Marekani kilichopo Nebraska 2011-13.

Aliambia kamati ya bunge kwamba, kwa mujibu wa alivyopokea mafunzo, atafuata amri ya rais kuhusu nyuklia - iwapo amri hiyo inafuata sheria.

Katika baadhi ya hali, alifafanua, "Ningesema 'Siko tayari kufanya hivyo.'"

Seneta mmoja alimwuliza: "Kisha, nini kitatokea?"

Bw Kehler alikiri: "Sijui".

Waliokuwa kwenye kamati hiyo waliangua kicheko.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii