Mhariri wa BBC ajiuzulu akilalamikia pengo kwenye mshahara na wanaume

Carrie Gracie

Mhariri wa BBC nchini China Carrie Gracie amejiuzulu kutoka wadhifa wake akilalamikia kutokuwepo kwa usawa wa mshahara na wafanyakazi wenzake wa kiume.

Kwenye barua Bi Gracie, ambaye amefanya kazi na BBC kwa zaidi ya miaka 30, ameilaumu BBC kwa ubaguzi katika malipo.

Alisema kuwa BBC inakumbwa na tatizo la kuaminiwa baada kufichuliwa kuwa theluthi mbili ya wanahabari nyota wanaolipwa zaidi ya pauni 150,000 walikuwa ni wanaume.

BBC inasema kuwa hakuna ubaguzi dhidi ya wanawake katika mpango wake wa ulipaji mishahara.

Bi Gracie alisema kuwa aliuacha wadhifa wake kama mhariri wa ofisi ya BBC mjini Beijing wiki iliyopita lakini bado atasalia kufanya kazi BBC.

Alisema atarudi kwa wadhifa wake wa zamani katika chumba cha habari cha televisheni ambapo anatarajiwa kulipwa sawa na wengine.

Mwezi Julai mwaka uliopita BBC ililazimsiwa kufichua mishahara ya wafanyakazi wote wanaolipiwa zaidi ya pauni 150,000 kwa mwaka.

Bi Gracie alisema alishangaa kugundua kuwa wahariri wawili wa kiume wa kimataifa wa BBC, walilipwa asilimia 50 zaidi kuliko wenzao wawili wa kike.

Mhariri wa Marekani Jon Sopel analipwa kati ya pauni 200,000-249,999, huku mhariri wa Mashariki ya Kati Jeremy Bowen akilipwa kati ya pauni 150,000-199,999.

Gracie hakuwa katika orodha hiyo ikimaanisha kuwa mshahara wake ulikuwa chini ya pauni 150,000.

Mada zinazohusiana