Apple: Kompyuta za Mac na simu za iPhone zimeathiriwa na kasoro

iPhones on display in an Apple store Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ni iPhone na Mac zinazotumia programu endeshi za kisasa zaidi pekee ambazo ni salama

Apple wamesema kwamba simu zote za iPhone, iPad na kompyuta za Mac zimeathiriwa na kasoro kubwa ambayo imegunduliwa katika kifaa muhimu ndani ya mitambo hiyo.

Ilibainika wiki iliyopita kwamba kampuni za teknolojia zimekuwa zikifanya juu chini kutatua kasoro ambazo zimepewa jina Meltdown na Spectre, ambazo zinaweza kuwapa wadukuzi fursa ya kuiba siri na habari muhimu kutoka kwa simu na kompyuta.

Kasoro hizo zinapatikana katika kisilikoni ambacho ndicho huendesha shughuli ndani ya kompyuta au simu wakati inapofanya kazi.

Mabilioni ya kompyuta, simu na tabiti kote duniani zimeathirika.

Apple nao pia wamethibitisha kwamba simu zao na kompyuta pia zimeathirika.

Kampuni hiyo imetoa vipande kadha vya programu vya kusaidia kuziba kasoro za Meltdown.

Apple wamesema hakuna ushahidi wowote kufikia sasa kwamba kasoro hizo zimetumiwa na wadukuzi.

Hata hivyo, wamewashauri wateja kwamba wanafaa kupakua vipande hivyo vya programu kutoka kwa mitandao ya kuaminika kuepuka kupakua programu ambazo zinaweza kuwa na kirusi.

Watu wanaotumia kompyuta za Mac wamekuwa kwa muda mrefu wakiamini kwamba mitambo yao ni salama zaidi kuliko wanaotumia mitambo mingine, mfano simu za Android au kompyuta zinazotumia programu endeshi za Microsoft.

Haki miliki ya picha Getty Images

Kasoro za Meltdown na Spectre flaws zinapatikana katika vipande vingi vya silikoni ambavyo hupatikana ndani ya kitovu cha kompyuta za kisasa ambazo ndizo huendesha shughuli muhimu za kompyuta.

Kwa ufupi, ndiyo kompyuta yenyewe. Kwa Kiingereza hufahamika kama 'microchip'.

Visilikoni ambavyo vina matatizo ni vile vilivyoundwa na kampuni za Intel na ARM, ambazo kwa pamoja ndizo huuza zaidi visilikoni vinavyotumiwa kwenye kompyuta duniani.

"Kompyuta zote za Mac na mitambo inayotumia iOS zimeathirika, lakini hatujafahamu kuhusu kutumiwa kwa kasoro hizo na wahalifu kufikia sasa," Apple walisema.

"Matatizo haya yanaathiri visilikoni vyote vya kisasa na yanaathiri karibu mitambo na vifaa vyote."

Apple walisema wametoa vipande vya programu vya kukinga dhidi ya Meltdown katika mfumo endeshi wa karibuni zaidi wa iPhone na iPad - iOS 11.2 na macOS 10.13.2 kwa ajili ya MacBook na iMac.

Meltdown haiathiri saa za Apple maarufu kama Apple Watch.

Programu ya kukinga dhidi ya Spectre, ambayo itawekwa kwenye mitambo kupitia kisakuzi cha Safari, itatolewa karibuni.

Google na Microsoft wametoa taarifa kuwafahamisha wateja ni mitambo gani imeathiriwa.

Google walisema simu zote za Android - ambazo ni 80% ya simu zote duniani - zimekingwa iwapo mteja alipakua na kuweka programu endeshi ya karibuni zaidi.

Microsoft wametoa vipande vya programu vya kutatua kasoro hiyo.

Kuuza hisa

Tatizo la kasoro hiyo kwenye microchip lilipobainika, na ikabainika kwamba limeathiri mabilioni ya simu na kompyuta, ilifahamika pia kwamba afisa mkuu mtendaji wa Intel Brian Krzanich aliuza hisa zake 245,000 katika kampuni hiyo Oktoba.

Hii ilikuwa wakati ambao Intel walikuwa wanafahamu kuhusu Meltdown na Spectre, lakini taarifa hizo zilikuwa hazijatolewa wazi kwa umma.

Intel wamesema kupitia taarifa kwamba uuzaji wa hisa za Brian haukuwa na uhusiano na kasoro hiyo. Wamesema uuzaji huo ulikuwa umepangwa mapema sana.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii