Mahathir Mohamad: Mzee wa miaka 92 anayetaka kuongoza Malaysia

Mahathir Mohamad in Putrajaya, Malaysia, on 30 March 2017 Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mahathir Mohamad amebaki kuwa na ushawishi sana siasa za Malaysia

Waziri mkuu wa zamani wa muda mrefu nchini Malaysia Mahathir Mohamad amechaguliwa kwa mara nyingine kuwania wadhifa huo, wakati huu akiwa na miaka 92.

Alichaguliwa Jumapili na muungano wa vyama vya upinzani kuwa mgombea wao katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika kabla ya Agosti.

Bw Mahathir alijiuzulu mwaka 2003 baada ya kushikilia wadhifa wa waziri mkuu kwa zaidi ya miongo miwili.

Iwapo atashinda, atakuwa miongoni mwa viongozi wakongwe zaidi duniani.

Miaka ya karibuni, amerejea kwenye siasa na amekuwa mkosoaji mkuu wa waziri mkuu wa sasa Najib Razak, ambaye amekabiliwa na tuhuma za kuhusika katika kashfa ya mabilioni ya dola inayohusisha hazina ya maendeleo ya serikali kwa jina 1MDB.

Mahathir alivunja uhusiano na chama tawala cha UMNO mwaka 2016 nakuanzisha chama kipya cha, Bersatu, ambacho kimejiunga na muungano wa upinzani wa Pakatan Harapan.

Ameungana na msaidizi wake wa zamani Anwar Ibrahim, ambaye mwenyewe alimfuta kazi 1998, kujaribu kumuondoa uongozini Najib Razak. Alikamatwa na kufungwa jela miaka sita kwa tuhuma za ulawiti na rushwa.

Ibrahim aliongoza upinzani uchaguzi wa 2013 na alifungwa jela tena mwaka 2015 kwa makosa anayosema yalichochewa kisiasa.

Upinzani umesema ukishinda utaomba msamaha kutoka kwa mfalme ndipo aweze kuruhusiwa kuwania wadhifa wa waziri mkuu.

Mada zinazohusiana