Manyunyu yazuia ndege isiyo na rubani kupaa Marekani

The SureFly drone had not been waterproofed, the company said Haki miliki ya picha Workhorse Group
Image caption Ndege hiyo SureFly haikuwa imeundwa kuzuia maji kuingia ndani yake

Safari ya kwanza iliyokuwa imesubiriwa kwa hamu na ghamu, ya ndege isiyo na rubani aina ya SureFly yenye uwezo wa kuwabeba abiria ilitibuka baada ya mvua ya manyunyu kunyesha.

Ndege hiyo haingepaa kwa sababu za kiusalama, kampuni iliyounda ndege hiyo ilisema.

Ndege hiyo ilikuwa imeidhinishwa kuanza kupaa na maafisa wa serikali wiki iliyopita.

SureFly, ndege inayotumia injini ya dizeli na umeme, inaweza kuwabeba watu wawili na inaweza kusafiri kwa umbali wa maili 70 (113km) bila kutua.

Bado kuna matumaini kwamba itaanza kufanya kazi hivi karibuni.

Ndege hiyo ni miongoni mwa teknolojia mpya ambazo zilikuwa zinaoneshwa kwenye maonyesho maarufu ya kila mwaka kuhusu teknolojia (CES) ambayo yamekuwa yakifanyika Nevada, Marekani.

Wanahabari walikuwa wamealikwa kushuhudia ikipaa kwa mara ya kwanza karibu na uwanja wa ndege wa jiji la Boulder.

Lakini safari hiyo ilifutiliwa mbali ghafla baada ya mvua ya manyunyu kuanza kunyesha.

Ndege kama hizo zimefanyiwa majaribio kwingine, maarufu zaidi ikiwa ndege ya kampuni ya Volocopter kutoka Ujerumani ambayo ilifanyia majaribio ndege yake Dubai Septemba mwaka jana.

Ndege hiyo ilikuwa na rafadha 18.

Ndege hiyo ya SureFly iliundwa na kampuni ya Workhorse Group yenye makao yake Ohio, na ina rafadha nane. Inaweza kubeba uzani wa kilo 181.

Workhorse waliambia BBC kwamba ndege hiyo haikuwa imeundwa kuzuia maji kuingia ndani, kwa sababu ilikuwa ya majaribio tu. Lakini walisema ndege zitakazoundwa baada ya hiyo zitakuwa na uwezo huo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii