Edward Lowassa akutana na Magufuli, amsifu kwa 'kazi nzuri' Tanzania

Lowassa na Magufuli Haki miliki ya picha Ikulu, Tanzania

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania ambaye pia ni Waziri mkuu wa zamani wa Tanzania Edward Ngoyai Lowassa amesifu kazi anayoifanya Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu, Bw Lowassa amesema hayo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo naye, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Bw Lowassa amempongeza Dkt Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya.

"Nimepata faraja sana kuja hapa Ikulu kuonana na Mhe. Rais, tumezungumza nae na nimempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, lazima tukiri anafanya kazi nzuri na anahitaji kutiwa moyo."

Bw Lowassa aliwania urais kupitia chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 lakini akashindwa na Dkt Magufuli aliyewania kupitia Chama cha Mapinduzi.

Ni hatua ambayo si ya kawaida kwa kiongozi huyo kumsifu Rais Magufuli kwani kwa muda amekuwa akikosoa utawala wake.

Kiongozi huyo wa upinzani nchini Tanzania, akizungumza na BBC mnamo mwezi Septemba mwaka 2016 , alieeleza wasiwasi wake kuhusu kile alichokitaja kama dalili za udikteta kwenye uongozi wa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli.

Haki miliki ya picha Ikulu, Tanzania

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu, Bw Lowassa amesema: "Moja kubwa ambalo ni la msingi sana ni la kujenga ajira, katika kuanza ujenzi wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hapo anajenga ajira.

"Na kwenye nchi yoyote inayoendelea suala muhimu ni kujenga ajira, Stiegler's Gorge ni kujenga ajira na mingine ya aina hiyo, lazima kuwepo na kipaumbele cha kusema kwamba tunajenga ajira, jingine ni la elimu, ni muhimu sana, hauwezi kuacha elimu katika mambo yako unayofanya, hili nalo lazima lisemwe vya kutosha, kwa kweli nakushukuru Mhe. Rais, you made my day" .

Huwezi kusikiliza tena
Lowassa: Kuna dalili za ‘udikteta’ serikali ya Magufuli Tanzania

Dkt Magufuli amesema Lowassa ni mwanasiasa mzuri kwani hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita ambao naye aligombea kiti cha Urais, hakuwahi kumtukana.

Amemshukuru "kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali".

Haki miliki ya picha Ikulu, Tanzania

"Lowassa ameniomba mara nyingi nikutane nae, na leo nimekutana nae, tumezungumza mambo mengi, ameniambia ya kwake na mimi nimemwambia ya kwangu, kwa ujumla Lowassa ni mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fulani walifanya mambo mazuri, na mimi napenda kumpongeza Lowassa ambaye kama alivyosema hapa kuwa tumefanya mambo mazuri mengi."

Haki miliki ya picha Ikulu, Tanzania

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii