Masaibu yaliyompata mfanyabiashara Kisumu baada ya uchaguzi Kenya

Image caption Masaibu yaliyompata mfanyabiashara Kisumu baada ya uchaguzi Kenya

Kila baada ya miaka mitano uchaguzi wa Urais nchini Kenya huleta furaha na majonzi kwa baadhi ya wanaopiga kura.

Kuna wale husherehekea mtu wao anaposhinda, na majonzi kwa wale mgombea wao anabwagwa chini.Ushindi pia wakati mwingine huleta huzuni hasa pale mtu anavamiwa kwa sababu ya kabila lake kwani ukabila umekita mizizi katika uchaguzi wa Kenya.Katika uchaguzi wa Urais mwaka uliopita, Uhuru Kenyatta hatimaye alitangazwa mshindi wa marudio ya uchaguzi wa Urais wakati kesi dhidi yake iliyowasilishwa mahakama ya juu zaidi ilitupiliwa mbali na Jaji Mkuu David Maraga.

Image caption Masaibu yaliyompata mfanyabiashara Kisumu baada ya uchaguzi Kenya

Mjini Kisumu mfanya biashara Joseph Kikwai wa chama cha Jubilee ni baadhi ya waliofurahia matokeo hayo. Lakini wafuasi wa chama cha upinzani cha NASA hawakupokea matokeo hayo kwa uzuri.

Kikwai, ambaye anatoka eneo la bonde la ufa, ameishi mtaa wa Kondele kwa miaka 18 mpaka akaamua kujenga nyumba yake huko kwani alijiona yuko nyumbani, na wala hakudhania siku moja angetendewa unyama na wakaazi wa huko.Lakini hayo hatimaye yalimpata wakati wafuasi wa NASA waliojawa na hasira waliamua kuchoma nyumba yake na kila kitu humo kwa sababu yeye ni mtu wa Jubilee na ni wa kabila la Kalenjin.``Nilipashwa habari na jirani aliponipigia simu nyumba yangu inachomwa na watu zaidi ya mia moja wakiwa wamebeba mapanga na silaha zingine hatari,'' anasema Kikwai.

Image caption Masaibu yaliyompata mfanyabiashara Kisumu baada ya uchaguzi Kenya

``Kidogo akili iruke lakini nikajikaza kiume, nikaanza kuelekea kwangu nijionee mwenyewe hasara hiyo. Haikuwa rahisi kufika kwangu kwa sababu barabara ziliwekwa vizuizi vya mawe na majambazi ambao walikua wanaamuru kila mtu atoe shillingi hamsini aruhusiwe kupita na kulikuwa na vizuizi zaidi ya vinne.

``Kufika kwangu sikuamini macho yangu. Nyumba yote imechomwa na mali zaidi ya millioni ishirini kuteketezwa.''

Kikwai anaeleza magunia ya mahindi 1,264 na maharagwe magunia 560, magari yake mawili na duka lake yalibakia kuwa jivu.Jitihada za kuhusisha polisi kutoka kituo cha Kondele hazikufua dafu kwa sababu mkuu wa kituo hicho waliamua kutotoka kutokana na habari za majambazi walikuwa wanapanga kuchoma kituo hicho.

Image caption Masaibu yaliyompata mfanyabiashara Kisumu baada ya uchaguzi Kenya

``Nimeumia kwa sababu ya kabila langu, natoka eneo la bonde la ufa anakotoka naibu wa Rais William Ruto lakini ajabu ni kwamba hakuna mkuu yeyote wa Jubilee amenipigia simu ama kuniuliza nataka usaidizi wa aina gani.

Namuomba Ruto na Rais Kenyatta wanisaidie kwa sababu nimeteswa kwa kuwa mfuasi wa Jubilee.'

Bahati nzuri siku hiyo familia yake, mke na watoto wanne hawakuwepo nyumbani.``Ilinibidi nitumane nguo zingine kwetu Kericho tuweze kubadilisha mavazi,'' asema Kikwai.Sasa ameanza maisha upya kwa kukomboa nyumba ya chumba kimoja anachokilipia sh5000 kila mwezi. Familia iko kwao Kericho.``Siamini ni mimi ninaishi hivyo kama kijana mdogo ameanza maisha. Ninapanga niuze hii ardhi nihame kabisa hapa. Siwezi kuishi na maadui hata kidogo kwa sababu sijui wananipangia nini tena,'' Kikwai anasema kwa hasira na huzuni pia, akikashifu wakuu wa Jubilee kwa kutomsaidia.