Picha ya mvulana iliyowaweka taabani H&M

Composite image of The Weeknd and a screengrab from the H&M website Haki miliki ya picha Getty Images/H&M

Wasanii na wachezaji mashuhuri duniani wamekosoa hatua ya kampuni ya mavazi na mitindo ya H&M kuweka tangazo la mvulana mweusi akiwa amevalia fulana yenye ujumbe ambao umefasiriwa kuwa wa ubaguzi wa rangi.

Fulana hiyo ya rangi ya kijani ilikuwa na ujumbe "coolest monkey in the jungle", kwa maana ya tumbili mtanashati au bora zaidi porini.

Mwanamuziki Diddy na mchezaji wa Manchester United Romelu Lukaku wamechukua hatua ya kupakia picha zenye ujumbe mbadala.

Mwanamuziki Abel Makkonen Tesfaye, maarufu kama The Weeknd, amesema hatafanya kazi tena na kampuni ya mavazi na mitindo ya H&M baada ya tangazo hilo.

The Weeknd amesema tangazo hilo limemuacha na "mshangao na aibu kubwa".

Mwanamuziki huyo awali amewahi kuuza bidhaa zenye nembo yake kupitia H&M na pia kuwatangazia bidhaa zao.

Ameandika kwenye Twitter kwamba amekerwa sana na picha hiyo.

H&M wamesema: "Tunasikitika sana kwamba picha hiyo ilipigwa, na tunajutia sana kwamba ilisambazwa.

"Kwa hivyo, tumeagiza iondolewe kutoka kwenye majukwaa yetu yote, na kwamba fulana hizo zisiuzwe tena."

Haki miliki ya picha H&M website

Rapa na produsa Diddy aliongeza ujumbe wa "coolest king in the world" (mfalme bora zaidi duniani).

Diddy aliandika kwenye Twitter: "Weka heshima kiasi".

Lukaku aliweka ujumbe wa "black is beautiful" (weusi ni maridadi) na kuandika "Wewe ni mwanamfalme na utakuwa mfalme karibuni."

Mchezaji wa mpira wa kikapu LeBron James aliweka ujumbe "King of the world" (Mfalme wa Dunia) na kumvika mvulana huyo taji.

Aliandika: "Sisi Wamarekani Weusi lazima kila wakati tutahitajika kuruka vizuizi, kuwathibitishia watu kwamba wamekosea na kutia bidii hata zaidi kuthibitisha kwamba tunastahiki".

Wengine wamekuwa wakizungumzia picha hiyo mtandaoni.