Sadfa gani umeme kukatika siku moja Kenya miaka miwili?

Tumbili alilaumiwa baada ya umeme kupotea maeneo mengi Kenya Juni 2016 Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Tumbili alilaumiwa baada ya umeme kupotea maeneo mengi Kenya Juni 2016

Wakenya mtandaoni bado wanazungumzia kisa cha jana jioni ambapo umeme ulikatika katika maeneo mengi nchini humo na kutumbukiza taifa hilo katika giza totoro.

Taifa jirani la Uganda pia lilikumbwa na tatizo sawa.

Jambo la kushangaza ni kwamba tarehe sawa na hiyo mwaka jana, mnamo 9 Januari, 2017, umeme ulipotea katika maeneo mengi nchini Kenya.

Shirika la kusambaza umeme Kenya, Kenya Power, limesema tatizo la jana lilisababishwa na hitilafu za kimitambo.

Maeneo mengi umeme ulirejea mwendo wa saa nne usiku, lakini Jumatano asubuhi bado kuna maeneo ambayo hayakuwa na umeme.

Kisa kinachokumbukwa sana ni cha Juni mwaka 2016 ambapo tumbili alilaumiwa kwa kusababisha umeme kukatika jijini Nairobi na maeneo mengi jirani.

Shirika la kuzalisha umeme KenGen lilisema tumbili huyo aliangukia transfoma katika kituo cha kuzalisha umeme cha Ndenderu eneo la Gitaru, kaskazini mwa Nairobi.

Umeme ulipotea kwa karibu saa nne kabla ya tatizo hilo kutatuliwa.

Tumbili huyo alinusurika na kuchukuliwa na maafisa wa Huduma kwa Wanyamapori.

Wakenya wamekuwa wakitania kukatika kwa umeme jana huku wakiikosoa Kenya Power. Wengine bado wanakumbuka kisa cha tumbili.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii