Kenya Airways yazindua safari za moja kwa moja hadi Marekani

Ndege ya Kenya Airways

Shirika la ndege la Kenya, Kenya Airways, limezindua uuzaji wa tiketi za safari ya kwanza kabisa ya ndege zake za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi Marekani.

Shirika hilo linapanga kufanya safari yake ya kwanza mnamo 28 Oktoba, hatua itakayoifanya Kenya Airways kuwa shirika la kwanza kutoka Afrika Mashariki kuwa na safari za moja kwa moja Marekani.

Ndege za shirika hilo litakuwa zinafasiri moja kwa moja hadi uwanja wa ndege wa JFK, New York.

Tiketi za kawaida zinauzwa Sh89,000 ($890).

Meneja Mkurugenzi wa Kenya Airways Sebastian Mikosz akizungumza wakati wa uzinduzi huo amesema safari hizo zitawafaa sana katika mpango wake wa ukuaji.

"Huu ni wakati wa kusisimua sana kwetu. Mpango huu unaingiana vyema na mpango wetu wa kuvutia abiria kutoka kwa mashirika na kampuni mbalimbali pamoja na watalii wa hadhi kufika Kenya na Afrika," amesema.

Image caption Mwenyekiti wa bodi ya Kenya Airways Michael Joseph

Kenya Airways itafanikisha safari hizo kwa ushirikiano na shirika la Delta Airlines la Marekani.

Mambo muhimu kuhusu safari hiyo:

  • Safari hiyo itachukua saa 15 kutoka New York hadi Nairobi na saa 14 kutoka Nairobi hadi New York.
  • Shirika hilo limesema litatumia marubani wanne na wahudumu 12 wa ndege.
  • Safari yote itatumia tani 85 za mafuta.
  • Shirika hilo litatumia ndege zake za kisasa aina ya Boeing 787 Dreamliner ambazo huwabeba abiria 234.
  • Ndege za kwenda Marekani zitaondoka JKIA Nairobi saa 23:25 na kufika JFK kesho yake saa 06:25.
  • Ndege za kurudi Nairobi zitaondoka New York 12:25 na kutua JKIA saa 10:55 kesho yake.

Masharti

Kwa mujibu wa Bodi ya Utalii Kenya, Kenya hupokea watalii 100,000 kutoka Marekani kila mwaka na safari hizo zinatarajiwa kuifanya nafuu kuzuru Kenya kwa kupunguza muda wa kusafiri na gharama.

Image caption Wahudumu wa Kenya Airways wakati wa uzinduzi huo

Kuzinduliwa kwa safari hizo ni matunda ya mashauriano ya muda mrefu kati ya Kenya na serikali ya Marekani.

Kenya ilipewa masharti ya kuimarisha usalama, ikiwa ni pamoja na kuwatenganisha abiria wanaotua na wanaoondoka, kufanya salama njia za safari ya ndege na pia kuweka ua katika uwanja wa ndege wa JKIA.

Kenya ilipewa hadi ya Kiwango cha Kwanza kutoka kwa Shirika la Safari za Ndege la Marekani Februari mwaka jana na kuifungulia njia Kenya Airways kufanya safari za moja kwa moja.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii