Wanandoa matatani kwa utesaji familia

Watuhumiwa mtu na mkewe Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Watuhumiwa mtu na mkewe

Polisi nchini Marekani wanawashikilia watu wawili baada ya kugundulika kwa watu 13 wanaodaiwa kufichwa ndani ya nyumba yao, huku baadhi yao wakiwa wamefungwa pingu vitandani zenye minyororo yenye kufuli.

Wanandoa wawili David Allen Turpin mwenye umri wa miaka 57 na Louise Turpin miaka 49 wanashikiliwa kwa makosa ya kuwatesa na kuwatia watoto hatarini.

Watu 13, wenye miaka kati ya miwili na 29, walikutwa ndani ya nyumba ya wanandoa hao katika kitongoji cha Perris Kusini Mashariki mwa Los Angeles na wanaaminika kuwa ni ndugu.

Maafisa wa usalama nchini humo, walipata taarifa kutoka kwa mmoja ya waathirika, ambaye alifanikiwa kutoroka siku ya Jumapili na kutoa taarifa kupitia namba ya dharura, kutoka katika simu aliyoikuta ndani ya nyumba hiyo.

Polisi wamesema mtoto huyo wa kike aliyekuwa akionekana kama ana miaka 10, na aliyedhoofu, amedai kuwa ndugu zake 12 bado wanashikliliwa na wazazi wao.

Baadaye maafisa wa polisi walipofika katika eneo hilo waligundua watoto hao kadhaa wakiwa na pingu vitandani na wengine kufungwa kufuli katika chumba chenye giza, kilichojaa harufu.

Hata hivyo, polisi wamesema mara tu baada ya kukamatwa wazazi wa watoto hao hawakuweza kutoa sababu kwanini walifanya jambo hilo.

Jirani zao nao wanasema ni nadra sasa walikuwa wakiwaona watoto hao.

Waathirika hao wote sasa wanaendelea kupata matibabu hospital.