Kunguni wagunduliwa ndege ya shirika la Uingereza

Ndege ya British Airways Haki miliki ya picha AFP

Waziri wa uchukuzi wa ndege nchini Ghana Cecelia Dapaah amelitahadharisha shirika la ndege la Uingereza, British Airways, kwamba huenda likaadhibiwa vikali.

Hii ni baada ya kunguni kugunduliwa katika baadhi ya ndege za shirika hilo.

Gazeti moja la Uingereza wiki hii liliripoti kwamba ndege moja ya BA ilizuiwa kuondoka kutoka uwanja wa ndege wa Heathrow mjini London kuelekea Accra baada ya kunguni kugunduliwa wakitambaa kwenye viti vya ndege hiyo.

Gazeti la The Sun lilichapisha habari kuwa wahudumu wa ndani ya ndege hiyo walipigwa na butwaa walipowaona kunguni wengi tu ndani ya ndege na kulazimu kuahirishwa kwa safari yao.

Wahudumu hao walizua taharuki walipokurupuka nje badala ya kuwaelekeza wasafiri kuingia ndani ya ndege hiyo.

Shirika hilo la ndege limejitetea likisema tukio hilo sio la kawaida na kwamba ndege hiyo haikuruhusiwa kuondoka uwanja wa ndege na haikufika mjini Accra.

Shirika hilo limesema limejitolea kutoa huduma ya hali ya juu kwa abiria wake.

Shirika la BA limehudumu nchini Ghana kwa miaka 80.

Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari mapema leo, shirika hilo la British Airways limesema kuwa limewatuma wataalamu wa kukabili ueneaji wa wadudu hao kulishughulikia suala hilo kikamilifu.

Haki miliki ya picha AFP

Licha ya maelezo hayo, waziri anayesimamia usalama wa anga nchini Ghana Bi Dapaah ameionya British Airways kuwa huenda hatua za kinadhamu zikachukuliwa dhidi yake iwapo tukio hilo halitakabiliwa haraka.

Tukio hilo la aibu ndilo la hivi punde zaidi kuikumba British Airways ambaye kwa mtazamo wa wengi imeathirika vibaya kutokana na kudorora kwa viwango vyake vya huduma kwa wateja.

Shirika hilo la ndege la Uingereza British Airways huwa halina ushindani mkali katika safari kati ya mji mkuu wa Ghana Accra na London.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii