Wanawake wadaiwa kubakwa baada ya kujifungua hospitalini Kenya

Wadi Hospitali ya Kenyatta Haki miliki ya picha AFP/Getty

Waziri wa afya nchini Kenya Dkt Cleopha Mailu ameamrisha uchunguzi kufanywa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta baada ya wanawake waliojifungua kudai kwamba wanadhalilishwa kingono.

Taarifa zilizoenezwa kwenye mitandao zinadai kina mama waliojifungua wamekuwa wanashambuliwa na baadhi ya wafanyikazi wakati wakienda kwenye chumba cha watoto wachanga kuwanyonyesha watoto wao.

Chumba hicho cha watoto huwa ghorofa tofauti na wadi za wanawake waliojifungua.

Wasimamizi wa hospitali hiyo wamesema hawajapokea malalamiko yoyote.

Yote yalianza baada ya ujumbe kuandikwa aktika ukurasa wa Facebook kwa jina Buyer Beware ambao mara nyingi hutumiwa kuwatahadharisha wateja na wanunuzi wa bidhaa na huduma.

Ujumbe uliwatahadharisha kina mama wanaojifungulia katika hospitali hiyo kwamba wamo hatarini ya kudhalilishwa kingono na baadhi ya wafanyakazi wa hospitali hiyo.

Wanawake wengine walichangia na kudai wamewahi kudhalilishwa au jaribio kufanywa, au jamaa na marafiki zao wakadhalilishwa.

Wengi wanadai kina mama waliojifungua waliviziwa wakiwa njiani kuelekea chumba hicho cha kunyonyeshea watoto au wakirudi chumba chao baada ya kunyonyesha.

Baadhi ya wanaodaiwa kunyanyaswa kingono, ujumbe unasema, walitendewa kitendo hicho siku chache baada yao kujifungua kupitia upasuaji.

Waziri Mailu ameagiza uchunguzi wa dharura kufanyika na ripoti kamili kuwasilishwa kwake kufikia Jumatatu.

Afisa mkuu mtendaji wa hospitali hiyo Lily Koros amesema hakuna mwanamke hata mmoja aliyewahi kulalamika kwamba alidhalilishwa kingono hospitalini humo.

Amesema hospitali hiyo huwa chini ya uangalizi wa kamera za usalama (CCTV) wakati wowote na hakuna kisa hata kimoja kilichogunduliwa.

Amewataka walio na habari kupiga ripoti kwa maafisa wa hospitali au polisi.

Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Wanawake 100 hujifungua kila siku hospitali ya Kenyatta

Hospitali ya taifa ya Kenyatta, Nairobi huwahudumia kina mama takriban 100 wanaojifungua kila siku.

Watoto waliozaliwa huwekwa chumbani ghorofa ya kwanza nao wanawake kwenye wodi za kujifungulia kwenye ghorofa ya chini.

Maswali sasa yameanza kuulizwa kuhusu muundo na mpangilio wa vyumba katika hospitali hiyo ambao huwalazimu kina mama waliojifungua kupanda ngazi au lifti kwenda kuwanyonyesha watoto wao, ikizingatiwa kwamba baadhi hujifungua kupitia upasuaji.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii