Mwanaanga Mwafrika-Mmarekani 'azuiwa' kuweka historia anga za juu Marekani

Dr Jeanette Epps Haki miliki ya picha NASA

Mtaalamu wa anga za juu nchini Marekani Jeanette Epps ameondolewa kutoka kwenye safari inayotarajiwa hivi karibuni ya kwenda Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (ISS) miezi michache kabla ya safari hiyo kufanyika.

Dkt Epp angekuwa Mwafrika-Mmarekani wa kwanza kujumuishwa miongoni mwa wahudumu wa kituo hicho.

Angesafiri anga za juu akitumia roketi ya Urusi kwa jina Soyuz mwezi Juni.

Lakini badala yake, ameondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na mwanaanga mwingine.

Shirika la anga za juu la Marekani Nasa halijatoa sababu zozote za kuondolewa kwake lakini limesema huenda akazingatiwa katika safari nyingine siku zijazo.

Jeanette Epps, mzaliwa wa Syracuse, alihitimu shahada ya udaktari katika uhandisi wa anga za juu mwaka 2000.

Baada ya kufuzu, alifanya kazi katika maabara kwa miaka miwili kabla ya kuajiriwa na shirika la ujasusi la Marekani, CIA.

Alifanya kazi kama afisa wa ujasusi wa kiufundi kwa miaka saba kabla ya kuteuliwa kuwa katika kundi la wanaanga wa Nasa mwaka 2009.

Alipokuwa na CIA, aliwahi kutumwa kufanya kazi Iraq.

Haki miliki ya picha NASA
Image caption Mzaliwa huyo wa Syracuse angesafiri anga za juu Juni
Haki miliki ya picha NASA
Image caption Nafasi ya Dkt Epps itachukuliwa na Serena Auñón-Chancellor, ambaye amefanya kazi na wahudumu wa ISS Urusi

Katika mahojiano na jarida la Elle mwaka jana, Dkt Epps alisema: "Najawa na furaha sana kufikiria kwamba nitaenda anga za juu, kiasi kwa sababu nailinganisha na kwenda eneo la vita.

"Yote mawili ni hatari, kwangu, sina shaka: Heri kuwa katika hatari za anga za juu kuliko kurejea vitani."

Aliongeza: "Watu wanaporejea kutoka anga za juu, huwa naona jinsi wanavyotaka sana kurudi huko."

Dkt Epps alipangiwa kuruka kwa roketi kutoka Baikonur, Kazakhstan, pamoja na Mjerumani Alexander Gerst na kamanda wa safari hiyo Mrusi Sergei Prokopev.

Nasa hawajatoa sababu yoyote ya kuondolewa kwake kutoka safari hiyo ya Expedition 56/57.

Kupitia taarifa, wamesema atarejea kazini kituo cha Nasa cha Houston kufanya kazi ya afisini.

Atakayechukua nafasi yake, Dkt Serena Auñón-Chancellor, ni daktari wa matibabu kutoka Fort Collins, Colorado. Aliwahi kukaa miezi tisa akisaidia juhudi za matibabu kwa wahudumu wa ISS Urusi.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii