Mnyarwanda Areruya Joseph ashinda tuzo kuu mbio za baiskeli Afrika

Areruya Joseph

Areruya Joseph amekuwa Mwafrika wa pili kushinda shindano la Latropicale Amissa Bongo ambalo ndilo la kwanza kubwa kwenye kalenda ya mashindano ya mbio za baiskeli barani Afrika.

Mashindano yalidumu kwa siku saba, washindani wakizunguka maeneo tofauti ya nchi ya Gabon.

Kwa ujumla Areruya alishinda mbio hizo akimzidi mpinzani wake mkuu, Mjerumani Holler Nikodemus, kwa sekunde 18.

Nikodemus alikuwa anawakilisha timu ya Bike Aid ya Ujerumani.

Mwafrika wa kwanza kunyakua ubingwa wa mashindano hayo alikuwa - Nathanael Berhane kutoka Eritrea akichezea timu ya Europcar inayoshiriki mashindano ya baiskeli barani Ulaya.

Haki miliki ya picha Hisani
Image caption Areruya akiwa na Rais wa Gabon Ali Bongo Ondimba (pili kushoto)

Areruya Joseph, 23, mwishoni mwa mwaka uliopita alishinda shindano la Tour of Rwanda ambalo ni la pili kwenye kalenda ya shirikisho la mchezo wa mbio za baiskeli barani Afrika na ameorodheshwa mchezaji bora wa pili barani Afrika.

Mada zinazohusiana