Wanaharakati waandamana Nairobi kutetea usawa wa jinsia

Wanawake

Wanaharakati kutoka mashirika mbali mbali ya kijamii nchini Kenya wameandamana jijini Nairobi kuishinikiza serikali kutekeleza kifungu cha katiba kinachotaka asasi za serikali ziwe na usawa wa kijinsia.

Maandamano hayo yameandaliwa wakati ambapo rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuunda baraza la mawaziri.

Waandamanaji hao wamesema kwamba kati ya nafasi 22 katika baraza la mawaziri, wanawake wanafaa watengewe nafasi 9.

Bw Kenyatta kufikia sasa amewateua wanaume pekee miongoni mwa mawaziri aliowateua.

Mmoja wa waandalizi wa mandamano hayo Mercy Jelimo amesema wanawake wanafaa kuachiwa nyingi ya nafasi zilizosalia za mawaziri.

Katiba ya Kenya inasema katika uteuzi wa viongozi na wanachama wa asasi za umma, jinsia moja haifai kuwa na watu wanaozidi theluthi mbili.

Juhudi za kutekeleza sheria hiyo, hasa bungeni na katika asasi nyingine zimekumbana na pingamizi.

Waandamanaji hao ambao walikuwa zaidi ya 400 walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe tofauti.

Kwa sasa wanawake katika Bunge la Kenya ni asilimia 19 ambayo ni idadi ndogo sana ikilinganishwa na asilimia 30 inayohiyohitajika kikatiba.

Katika kanda hii, Rwanda inaongoza kwa kuwa na wanawake 63.8% katika bunge lake.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii