Matumaini ya wakimbizi mwaka 1 tangu Marekani iwafungie milango

Hassan Nassor mkimbizi katika kambi ya Daadab Kenya
Image caption Hassan Nassor akiwa na mkewe na wanawe watano katika kambi ya wakimbizi Daadab Kenya

Katika mwaka ambao Donald Trump ameshikilia uongozi wa Marekani, wengi katika mojawapo ya kambi kubwa za wakimbizi duniani wanauliza iwapo Amerika imewapa mgongo.

Takriban wakimbizi laki mbili unusu wa kisomali wanaishi katika kambi ya Daadab, kaskazini mashariki mwa Kenya.

Lakini misaada kutoka nje inapungua, serikali ya Kenya inataka kuifunga kambi hiyo na utawala wa rais Trump umepiga marufuku watu wa mataifa sita ikiwemo Somalia kuingia nchini Marekani.

Mamia ya wakimbizi katika kambi hiyo kama Muhideen Hassan Nassor waliokuwa na matumaini ya kwenda Marekani, wameathirika.

Nyumbani kwa Hassan Noor, anaonekana akipiga gumzo na wanawe.

Yeye, mkewe na wanawe watano ni miongoni mwa watu waliathiriwa na hatua ya rais Trump.

Alianza utaratibu wa kutafuta hifadhi Marekani miaka saba iliyopita na alifanikiwa mwaka jana.

Siku tatu kabla ya kufunga safari kuelekea Marekani, Rais Trump akatangaza mafuruku iliyoathiri maelfu wakimbizi kutoka nchi sita ikiwemo Somalia.

'Wakati rais Trump akisherehekea kuapishwa kwake na sisi tulikuwa tunasherehekea kufaulu kupata hifadhi Marekani…lakini tukaambiwa hatuendi. Ni kama mtu ambaye amepita mtihani lakini wakati anasherehekea umwambie hapana hujafaulu', anasema Noor.

Image caption Takriban wakimbizi laki mbili unusu wa kisomali wanaishi katika kambi ya Daadab,

Hatahivyo Noor bado ana matumaini kuwa ndoto yake ya kupata hifadhi Marekani itatimia. Anasema kilicho muhimu zaidi ni hali ya baadaye ya watoto wake.

Ameongeza, 'Naiomba tafadhali Marekani ibadili msimamo, sisi sio wahalifu, sisi sio magaidi, kama tungekuwa watu aina hiyo, hatungeishi hapa kwa miaka ishirini na saba'.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR, linasema katika kambi za Daadab lina zaidi ya wakimbizi elfu moja wanaohitaji hifadhi kwa dharura.

Idadi inayotarajiwa kuongezeka kwani Marekani ndiyo nchi iliyokuwa inaongoza katika kuwapa hifadhi wakimbizi wa Somalia.

Picha zote/Peter Njoroge, BBC

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii