Tumbili 'waumbiwa' katika maabara ya China

Zhong Zhong na Hua Hua

Chanzo cha picha, Qiang Sun

Maelezo ya picha,

Zhong Zhong na Hua Hua

Tumbili wawili wameumbwa katika maabara nchini China, kwa kutumia mbinu sawa na iliyotumiwa kumuumba kondoo maarufu kwa jina Dolly.

Shughuli hiyo ambayo huhusisha kiumbe kuumbwa kutoka kwa kiumbe mwingine bila kujamiiana kwa Kiingereza hufahamika kama 'cloning'.

Hatua hiyo imetoa matumaini kwamba huenda teknolojia hiyo ikatumiwa siku za usoni kwenye binadamu.

Tumbili hao wanaofanana na wenye mikia mirefu kwa majina Zhong Zhong na Hua Hua 'walizaliwa' wiki kadhaa zilizopita katika maabara moja nchini China.

Wanasayansi wanasema kuwa tumbili kama hao ambao wanafanana kinasaba watakuwa muhimu sana kwa matumizi katika utafiti kuhusu magonjwa yanayowaathiri binaadamu.

Lakini wakosoaji wanasema kazi hiyo inazua wasiwasi wa kimaadili kwa kuwa inauleta ulimwengu karibu na utengezaji wa binaadamu katika maabara.

Qianga Sun wa taasisi ya sayansi ya neva amesema kuwa tumbili hao watatumika kama kigezo cha utafiti wa magonjwa ya jeni ikiwemo saratani, yale ya metaboliki na matatizo ya kinga mwilini.

''Kuna maswali mengi kuhusu biolojia na maumbile ya tumbili ambayo yanaweza kufanyiwa utafiti kwa kutumia kigezo hicho," alisema.

Chanzo cha picha, Chinese Academy of Sciences

Maelezo ya picha,

Zhong Zhong alitengenezwa kwa kutumia uhamisho maalum wa chembe za seli

Zhong Zhong alizaliwa wiki nane zilizopita naye Hua Hua akazaliwa wiki sita zilizopita.

Wamepewa majina kwa kutumia lugha ya Mandarin (Kichina), kwa maana ya miongoni 'Taifa la China' na 'Watu wa China'.

Watafiti wanasema kuwa tumbili hao wanalishwa kwa kutumia chupa na wanakua kama kawaida.

Wanatarajia tumbili zaidi kuzaliwa kupitia maabara katika miezi michache ijayo.

Profesa Darren Griffin wa chuo kikuu cha Kent amesema kuwa mpango huo unaweza kuwa muhimu katika kuelewa magonjwa ya wanadamu, lakini pia unazua wasiwasi wa kimaadili.

Dolly aliweka historia miaka 20 iliyopita baada kutengenezwa katika maabara ya taasisi ya Roslin mjini Edinburgh.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa wanasayansi kufanikiwa kutengeneza mnyama wa jamii ya mamalia kutoka kwa seli ya kiwele.

Chanzo cha picha, Science Photo Library

Maelezo ya picha,

Dolly ni kondoo ambaye alikuwa mnyama wa kwanza kuundwa katika maabara miaka 20 iliyopita

Tangu wakati huo wanyama wengine wametengezwa kupitia maabara kwa kutumia njia kama hiyo ya kuhamisha chembe muhimu za seli wakiwemo ng'ombe, mbwa, paka, panya na nguruwe.

Hatua hiyo inashirikisha kuhamisha jeni kutoka kwa seli hadi katika yai ambalo lilitolewa jeni zake za DNA.

Hiyo husababisha kutengezeka kwa kiinitete ambacho huwekwa katika mnyama mwengine atakayembeba mtoto huyo.

Zhong Zhong na Hua Hua ndio vizazi vya tumbili wa kwanza waliozaliwa kupitia mfumo huo.

Mwaka 1999, kiinitete cha tumbili kiligawanywa mara mbili kwa lengo la kutengeza pacha wanaofanana.

Mmoja wa watoto hao wa tumbili waliozaliwa kupitia mfumo huo - kwa jina tetra- hutambuliwa kama tumbili wa kwanza aliyezaliwa kupitia maabara lakini hakushirikisha mfumo huo wa kuhamisha jeni.

Chanzo cha picha, CHINESE ACADEMY OF SCIENCES

Maelezo ya picha,

Hua Hua alizaliwa wiki sita zilizopita katika maabara ya Shanghai

Zhong Zhong na Hua Hua ni matokeo ya majaribio 79.

Tumbili wengine wawili waliundwa kupitia maabara kutokana na seli tofauti lakini wakafariki muda mfupi baadaye.

Daktari Sun alisema: "Tulitumia njia tofauti, lakini ni njia moja pekee iliofanikiwa. Tulijaribu mara kadhaa na kushindwa kabla ya kufanikiwa kuunda tumbili kwa kutumia njia ya maabara."

Maelezo ya picha,

Zhong Zhong na Hua Hua

Wanasayansi hao wanasema kuwa walifuata maagizo makali ya kimataifa kuhusu utafiti wa wanyama yaliyowekwa na taasisi ya kitaifa kuhusu afya nchini Marekani.

Mtafiti mwenza Dkt muming Poo, kutoka taasisi hiyo ya China mjini Shanghai alisema: "Tunafahamu kwamba tafiti za siku za usoni zinazotumia wanyama wasio tumbili popote dunia zitategemea iwapo wanasayansi watafuata maagizo makali ya kiimadili."