Trump: Palestina iliikosea heshima Marekani

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na rais Donald Trump pembezoni mwa mkutano wa kiuchumi mjini Davos Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na rais Donald Trump pembezoni mwa mkutano wa kiuchumi mjini Davos

Rais wa Marekani Donald Trump amehoji iwapo mazungumzo ya amani na Israel yataendelea , akiwalaumu Wapalestina.

Bwana Trump alisema kuwa taifa la Palestina liliikosea heshima Marekani kufuatia uamuzi wake uliozua utata wa kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.

''Marekani lazima ipewe heshima ama hatutaendelea na lolote'', aliambia maripota mjini Davos''.

Palestina inasema kuwa Marekani haiwezi kuwa mpatanishi asiyependelea upande wowote. Rais Mahmoud Abbas ametaja hatua ya rais Trump kutambua Jerusalem kuwa pigo la karne kwa upande wa Palestina.

Hatahivyo, akiwa na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika kongamano la kiuchumi la World Economic Forum, bwana Trump alisema: Israel imekuwa ikiunga mkono Marekani kwa hivyo kile nilichofanya kwa Jerusalem ni heshima.

"Tuliiondoa Jerusalem katika meza ya majadiliano, kwa hivyo hatutaizungumzia tena.Palestina bado haijakubali hilo''.

Akizungumza na Netanyahu , bwana Trump alisema: Ulishinda alama moja, na baadaye utalazimika kuachilia alama nyengine baadaye katika mazungumzo iwapo yatafanyika, sijui iwapo yataweza kufanyika.

Jerusalem ni mji ambao umekuwa katikati ya mzozo kati ya Israel na Palestina.

Israel inautambua mji wa Jerusalem kuwa moyo wake na mji wake mkuu, huku Palestina ikidai kuwa eneo la mashariki mwa Jerusalem ambalo lilikaliwa kimabavu na Israel katika vita vya mashariki ya kati vya 1967 ni mji mkuu wa taifa la siku za baadaye.

Hatua ya rais Trump kuutambua mji huo kuwa mji mkuu wa Israel ilivunja sera ya miongo kadhaa ya Marekani kuhusu kutopendelea upande wowote hatua iliopelekea jamii yote ya kimataifa kujitenga na uamuzi huo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii