Wachapishaji wa Red Pepper waahidi kutopunguza makali Uganda licha ya kupewa kitabu na Museveni

Wanahabari wakiandamana Uganda Mei 2013 Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Chama cha kutetea haki za waandishi kimewataka wanahabari kuwa makini kabla ya kuchapisha taarifa

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ametoa msamaha kwa wakurungezi wakuu na wahariri wa gazeti la Red Pepper nchini Uganda, lakini wahariri hao wameahidi kutobadilisha sana utendaji kazi wao.

Gazeti hilo lilifungiwa kufanya kazi tangu Novemba mwaka jana.

Rais Museveni amewaonya wahariri na wakurugenzi hao wa Red Pepper wawe wangalifu katika uandishi wao.

Wamekuwa kizuizini Luzira tangu Novemba kwa mashtaka kadhaa ya kuchapisha habari za kutishia usalama wa taifa, kashfa na za kuchukiza.

Msamaha huo wa Rais ulitokea baada ya wakuu wa gazeti hilo kukutana na Rais Yoweri Museveni katika ikulu yake ya Entebbe siku ya Jumanne usiku.

Rais amewasamehe wakurugenzi wakuu watano na wahariri wakuu watatu.

Kadhalika, aliliamuru jeshi la polisi kuondoka kwenye ofisi za gazeti hilo zilizokuwa zimefungwa tangu tarehe 21 mwezi wa Novemba 2017, walipokamatwa wakurugenzi na wahariri wa gazeti hilo.

Mmoja wa wakurugenzi wa Red Pepper, Arinaitwe Rugyendo amemwambia BBC Isaac Mumena mjini Kampala kwamba hawawezi kurejelea majukumu yao ya kawaida kwa sasa kwa sababu polisi bado wamezingira ofisi za gazeti hilo wakisubiri amri ya msamaha kwa maandishi.

Afisi hizo za gazeti la Red Pepper zinapatikana sehemu ya Namavye wilayani Mukono barabara kuu ya kutoka Kamapla kwenda Jinja.

"Kwa nini gazeti haliko mitaani? Ni kwa sababu amri ya maandishi ya rais, inatakiwa kwa mchakato wa kisheria, mara amri hiyo ya maandishi itakapofika polisi ndipo tutaanza kufanya kazi, mpaka sasa ofisi hazijafunguliwa ila tunaruhusiwa kufanya kazi na kuingia ofisi," alisema Bw Rugyendo Alhamisi.

"Leo tulikuwa na mikutano mbalimbali ya kufanya kazi ya toleo linalofuata."

Gazeti la Red Peper lilifungwa baada ya kuchapisha habari ambazo serikali inasema zinatishia usalama wa taifa na kikanda.

Mwandishi wa BBC Isaac Mumena anasema kilichoonekana kuwaudhi wakuu wa Uganda ni taarifa ya Red Pepper wakati huo iliyodai Rais Museveni anafanya njama ya kupindua rais Paul Kagame wa Rwanda, jambo linalokanushwa kata kata na serikali ya Uganda.

Pia kuwatuhumu nduguye rais Museveni Salim Saleh na waziri wa usalama wa taifa Jenerali Henery Tumukunde.

Katika kutoa msamaha rais Museveni aliwaonya wakurugenzi wakuu na wahariri wakuu wawe wangalifu na kufata maadili ya kazi yao wakati wanaporipoti.

Baada ya kuwapatia msamaha rais aliagiza wafanyakazi wake wa ikulu kuwapatia kitabu chake cha toleo la pili 'Sowing Mastard Seed' kila mmoja pamoja na hotuba yake aliyetoa mwaka jana chuo kikuu cha Makerere kuadhimisha siku ya aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela.

Viongozi wa Chama cha kutetea haki za wandishi wa habari nchini Uganda, UJUU, wamepongeza Rais Museveni kwa msamaha huo na kutowa wito kwa wandishi habari kuwa makini wanaporipoti.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Museveni aliwapa wakurugenzi na wahariri hao nakala za kitabu chake

Chama cha kutetea haki za wandishi habari nchini Uganda UJUU kimeonya wandishi habari, kufanya uchunguzi kabla ya kuchapisha taarifa zozote.

"Kwa hiyo tunawapa wito wajaribu kufanya uchunguzi wa kutosha pia wajaribu kufatia sheria zetu na maadili ya wandishi habari kuona kwamba tunafanya kazi mtido wa juu sana," alisema katibu mkuu wa chama hicho Stephen Ouma.

Wakurugenzi wakuu na wahariri wakuu wa gazeti la Red Pepper wameahaidi kwa rais na taifa kuanzia sasa watachapisha habari za weledi.

Baada ya agizo hilo la rais wafanyakazi wa gazeti hilo waliweza kuingia katika ofisi zao lakini haijulikani ni lini wataanza rasmi kuchapisha gazeti lao.

Hii ni kwa sababu vifaa vyao vya kufanyia kazi pamoja na kompyuta, kamera na simu vilitwaliwa na jeshi la polisi kwa upelelezi.

"Hatujapata vitenda kazi vyetu lakini jana jioni (Jumatano) mmoja wa mawakili wetu alitufahamisha kuwa alipigiwa simu na mmoja wa wapelelezi na kumufahamisha kuwa leo wengi wa wafanyakazi watapata simu zao, isipokuwa wale wanaokabiliwa na mashtaka," anasema Rugyendo.

Haki miliki ya picha AFP

Je, Red Pepper, wataendelea na kutoa ripoti zao moto moto zenye utata zinazowavutia wasaomaji wa gazeti hilo?

"Ndiyo tutarudi na wandishi wetu wa kuchapisha habari kama ilivyokuwa zamani ila ila kitu tunachokwenda kubadilisha ni kama vile nyoka, nyoka ni yule yule ana badilisha ngozi ," alisema.

"Tunakwenda kubadilisha ngozi yetu kidogo na kupiga msasa hapa na pale na kuondoa kidogo makali na kuboresha."

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii