Watu wanne wafariki katika mkasa wa moto mtaa wa Kijiji, Nairobi

Moto Langata Haki miliki ya picha HISANI

Mamia ya watu wamekesha nje usiku wa kuamkia leo Jumatatu, bila ya kuwa na mahali pa kulala, nchini Kenya, baada ya moto mkubwa kuteketeza nyumba zao katika mtaa wa Kijiji eneo la Langata, Nairobi.

Watu wanne wamethibitishwa kufariki.

Maafisa wa serikali wanasema nyumba 6,000 ambazo ni makao ya watu takriban 14,000 ziliharibiwa na moto huo.

Moto huo ambao chanzo chake bado hakijabainika ulizuka mwendo wa saa mbili jioni na kuenea kwa haraka.

Magari manne ya wazima moto yalifika eneo hilo kujaribu kuuzima moto huo lakini hazikuweza kuufikia kutokana na njia nyembamba mtaani humo.

Magari hayo yalijaribu kuuzima moto huo kutoka mbali lakini baadaye yakaishiwa na maji.

Image caption Moto huo uliharibu nyumba za familia takriban 6,000

Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Taifa ya Kukabiliana na Majanga anayeangazia mawasiliano Bw Pius Masai aliambia gazeti la kibinafsi la Nation kwamba walilazimika kuomba usaidizi zaidi.

Magari ya kuzima moto ya baraza la jiji yalifika baadaye, lakini wakazi waliwalaumu maafisa hao wa serikali kwa kuchelewa kufika eneo la mkasa.

Moto huo baadaye ulizimwa, ingawa moshi bado ulikuwa unafuka katika baadhi ya maeneo asubuhi.

Wakazi waliambia vyombo vya habari kwamba walipoteza mali ya mamilioni ya pesa, badhi wakipoteza biashara zao na wengine makazi.

Picha/Peter Njoroge na Judith Wambare, BBC

Mada zinazohusiana