Wahusika wakuu mpango wa kumuapisha Odinga kuongoza Kenya

Bw Musyoka na Bw Odinga
Image caption Bw Musyoka na Bw Odinga

Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga amekuwa akisisitiza kwamba ataendelea na mpango wake wa kuapishwa kuongoza Kenya baada yake kutangaza kwamba hamtambui Bw Uhuru Kenyatta kama kiongozi aliyechaguliwa kwa njia halali.

Anapanga kuapishwa tarehe 30 Januari. Wahusika wakuu wamekuwa akina nani?

Raila Odinga

Image caption Bw Odinga alihudumu kama Waziri Mkuu 2008-2013

Raila Amolo Odinga ni kiongozi wa muda mrefu Kenya ambaye amehusishwa na harakati za kupigania mageuzi ya kisiasa nchini humo.

Amewania urais nchini Kenya mara nne bila mafanikio, na ya tano ingawa alikuwa kwenye karatasi za kupigia kura, alisusia.

Aliwahi kuhudumu kama waziri mkuu wa Kenya, wadhifa ulioundwa kufuatia Mkataba wa Kitaifa ulioafikiwa kumaliza ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007-2008, ambapo aligawana mamlaka na Rais Mwai Kibaki.

Mwaka 2017, Bw Odinga alikuwa miongoni mwa viongozi watano waliojiita Pentagon ambao wanaongoza muungano wa umoja wa vyama vya upinzani, National Super Alliance (NASA).

Bw Odinga aliishi kukamatwa na kuachiliwa mara kwa mara tangu mwaka 1982 hadi 1991 kwa harakati zake za kupigania mageuzi wakati wa muhula wa pili wa utawala wa rais Daniel arap Moi.

Amekuwa akisema lengo lake kuu ni kufanikisha mageuzi ya kisiasa Kenya na pia kumaliza ufisadi.

Bw Odinga ni mwanasiasa anayesifika sana kwa ushawishi wake kisiasa na amekuwa katika mstari wa mbele kuunda vyama vya miungano na wanasiasa ambao, wengine wakati mmoja walikuwa mahasimu wake.

Agosti 2017, uchaguzi ulipofanyika, tume ya uchaguzi ilitangaza kwamba alikuwa ameshindwa na Rais Kenyatta.

Alipinga matokeo hayo Mahakama ya Juu na uchaguzi huo ukafutiliwa mbali na uchaguzi mpya kuandaliwa tarehe 26 Oktoba.

Lakini Bw Odinga alisusia uchaguzi huo akisisitiza kwamba mageuzi yalihitajika katika tume ya uchaguzi kabla ya uchaguzi huru na wa haki kufanyika.

Mahakama ya Juu ilipoidhinisha kuchaguliwa kwa Bw Kenyatta na baadaye akaapishwa tarehe 28 Novemba, Bw Odinga alisema kamwe kwamba hatamtambua kama kiongozi aliyechaguliwa na wananchi Kenya.

Kalonzo Musyoka

Image caption Bw Musyoka amewahi kuwa makamu wa rais Kenya

Kalonzo Musyoka ni kiongozi wa chama cha Wiper Democratic Movement of Kenya na kiongozi mwenza wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (Nasa).

Ni makamu wa rais wa zamani, ambaye alihudumu chini ya Rais Mwai Kibaki kati ya 2008 hadi 2013.

Alikuwa mgombea mwenza wa Bw Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa 2013 (Coalition for Reforms and Democracy - Cord) na tena mwaka 2017.

Aliwania urais mwaka 2007 kupitia chama cha ODM-Kenya lakini akashindwa.

Alikuwa amehudumu serikalini kama waziri wa mambo ya nje 1993 hadi 1998 na tena 2003 hadi 2004.

Alihudumu kama waziri wa elimu 1998 he na baadaye kama waziri wa utalii 2001 hadi 2002.

Musyoka alikuwa ameteuliwa kuwa waziri wa mazingira mwaka 2004 lakini 2005 akapinga rasimu ya katiba iliyokuwa inaungwa mkono na serikali ya Rais Mwai Kibaki na baadaye akafutwa kazi.

Amekuwa akisisitiza kwamba ni sharti Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto wakubali kushauriana na serikali la sivyo mambo 'yatakuwa mabaya'.

Musalia Mudavadi

Image caption Musalia Mudavadi ndiye makamu wa rais aliyehudumu muda mfupi zaidi Kenya

Musalia Mudavadi ni kiongozi wa Amani National Congress (ANC) na aliwania urais mwaka 2013 lakini akamaliza wa tatu nyuma ya Bw Odinga na Bw Kenyatta.

Amekuwa mmoja wa viongozi wenza wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (Nasa).

Bw Mudavadi ni mwanasiasa wa muda mrefu nchini Kenya ambaye anashikilia rekodi ya kuwa makamu wa rais aliyehudumu kwa muda mfupi zaidi tangu uhuru - miezi miwili.

Alihudumu kama naibu waziri mkuu mwaka 2008 hadi 2013.

Amewahi kushikilia nyadhifa mbalimbali katika baraza la mawaziri, zikiwemo Waziri wa Fedha chini ya Rais Daniel arap Moi.

Kwa muda mrefu, amekuwa akitazamwa kama watu walio katika nafasi nzuri ya kuwa rais nchini Kenya.

Moses Wetangula

Image caption Bw Wetangula amewahi kuhudumu kama waziri wa mambo ya nje

Ni mmoja wa viongozi wenza wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (Nasa) ambaye amekuwa kiongozi wa walio wachache Bunge la Seneti tangu 2013.

Amekuwa akihudumu katika Bunge la Seneti kama seneta wa jimbo la Bungoma, magharibi mwa Kenya.

Awali, alikuwa kiongozi mwenza katika muungano wa upinzani wa awali wa Coalition for Reform and Democracy (Cord) ambao Bw Odinga aliutumia kuwania urais mwaka 2013.

Bw Wetangula amekuwa kiongozi wa chama cha Forum for the Restoration of Democracy-Kenya (Ford-Kenya) tangu 2011 ambacho 2013 kilikuwa kwenye muungano wa Cord na mwaka 2017 katika muungano wa Nasa.

Alijiingiza katika siasa mwaka 2003 alipochaguliwa mbunge wa Sirisia, magharibi mwa Kenya na kuhudumu tangu 2012.

Alihudumu kama maziri msaidizi wizara ya mambo ya nje kati ya 2003 na 2008 ambapo aliteuliwa waziri wa mambo ya nje hadi 2012.

Aliteuliwa waziri wa biashara 2012 na kuhudumu hadi 2013.

Alikuwa mmoja wa wajumbe wakuu upande wa chama cha PNU chake Mwai Kibaki wakati wa mazungumzo yaliyoongozwa na Kofi Annan ya kumaliza mzozo wa baada ya uchaguzi wa 2017.

James Orengo

Haki miliki ya picha AFP/Getty

James Aggrey Bob Orengo ni wakili na mwanasiasa wa muda mrefu, ambaye alishiriki harakati za kupigania mageuzi ya kisiasa miaka ya 1980 na 1990 na aliwahi kufungwa jela wakati wa utawala wa Daniel arap Moi.

Alichaguliwa kuwa mbunge wa eneo la Ugenya akiwa na miaka 29, wakati huo akiwa mbunge wa umri mdogo zaidi kuchaguliwa. Alihudumu kama mbunge wa eneo hilo mara kwa mara.

Aliwania urais mwaka 2002 akitumia chama cha Social Democratic Party (SDP) lakini akamaliza wa nne.

Mwaka 2008, aliteuliwa waziri wa ardhi na kuhudumu hadi 2013.

Amekuwa akihudumu kama seneta wa Siaya tangu 2013.

Bw Orengo ni mmoja wa mawakili ambao walihusika sana wakati wa kesi ya Bw Odinga ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa tarehe 8 Agosti, 2017.

Mara kwa mara hutumiwa kutoa msimamo wa muungano wa upinzani wa Nasa.

Norman Magaya

Kwa sasa ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Muungano wa upinzani (NASA) ambaye amekuwa karibuni akitoa taarifa kuhusu mpango wa kumuapisha Bw Odinga.

Magaya ni wakili wa masuala ya katiba na haki za binadamu na amekuwa akifanya kazi ya uanasheria tangu 2012.

Alishiriki katika kikosi cha mawakili waliofanikiwa kuwasilisha kesi ya kupinga ushindi wa rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa Agosti 8, 2017.

Ni mhadhiri wa sheria katika chuo kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (CUEA).

Magaya alihudumu kama mmoja wa wakala wa Muungano wa Upinzani (NASA) katika uchaguzi wa Agosti.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii