UNHCR yashtushwa na wimbi la Wakimbizi DRC

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa pamoja na wa DRC Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa pamoja na wa DRC

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi UNHCR limesema limeshtushwa na mapigano yanayoendelea Mashariki mwa Demokrasia ya Congo, hivyo kusababisha wimbi kubwa la wakimbizi kutoka nchini humo wanaoingia katika nchi jirani kama vile Burundi, Tanzania na Uganda.

Maelfu ya watoto, wanawake na wanaume wameacha makazi yao huku mapigano dhidi ya makundi yenye silaha ya Mai Mai yakiendelea Kusini mwa Jimbo la Kivu.

Kwa mujibu wa Shirika la UNHCR, mpaka sasa, wakimbizi wapatao 1200 wameingia nchini Tanzania. Wakati huo huo, inaamika kwamba, kuna wimbi kubwa zaidi za wakimbizi ambao wapo Kivu Kusini wakiwa katika hali mbaya ya kukosa chakula na makazi.

"Katika wakimbizi 1200, 300 ni wanaume. Wanakuja kwa kwa kutumia boti, takriban wote wanakuja kwa boti, awali raia kutoka Congo walikuwa wanakuja kupitia Burundi, kwa miguu, hiyo ndio tofauti na wakimbizi wa sasa, wanapokelewa na serikali na UNHCR, na mashirika mengine, tunawapa malazi, chakula wanapewa, maji na vitu vyengine na dawa pia, wanapokelewa hapa, baadae wanaenda katika kambi ya wakimbizi ya Nyargusu," amesema Bi Joan Allison ni naibu mwakilisha wa UNHCR nchini Tanzania.

Bi Joan amesema, wakimbizi hao wamekuwa wakiingia nchini Tanzania kwa kutumia Ziwa Tanganyika, huku wakiwa wamechoka na baadhi wakiwa katika hali mbaya ya kiafya.

"Rasilimali ni chache kwa wakimbizi, mahitaji ni makubwa. Tunajitahidi kadri tunavyoweza lakini tunahitaji rasilimali zaidi iwapo hali itaendelea kuwa tete," amesema Joan.

Hata hivyo, imeelezwa kwamba, wimbi hili la wakimbizi, limeongeza changamoto ya upatikanaji wa malazi, maji na hata huduma za choo, huku wengine wakiwa hawana jinsi zaidi ya kulala katika sehemu zilizo wazi.

UNHCR imesema, hivi sasa inatafuta usaidizi wa chakula, maji na dawa katika maeneo ya kupokewa wakimbizi.

Mada zinazohusiana