Raila Odinga anafaa kujiita nani kwenye Twitter?

Odinga Haki miliki ya picha AFP/Getty

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga alipokuwa kiapo kuwa rais wa wananchi jijini Nairobi Jumanne, mjadala ulizuka kuhusu wadhifa wake.

Alikuwa amekula kiapo kuwa 'Rais wa Kenya' au 'Rais wa Wananchi nchini Kenya'?

Muda haukupita kabla ya utata huo kujitokeza katika maelezo kuhusu ukurasa wake wa Twitter @RailaOdinga.

Awali, ukurasa huo ulikuwa na maelezo kwamba yeye ni kiongozi wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance (Nasa).

Muda mfupi baada yake kukamilisha kula kiapo, maelezo yalibadilishwa na akawa 'Rais wa Jamhuri ya Kenya.'

Hapo ndipo utata ulipoanza, kwani Rais Uhuru Kenyatta hujitambulisha pia kama Rais wa Jamhuri ya Kenya.

Haki miliki ya picha TWITTER

Muda baadaye, alibadilisha na kuwa kiongozi wa Nasa.

Baadaye usiku, alibadilika na kuwa "Aliyeapishwa kuwa Rais wa Wananchi mnamo 30/1/2018'.

Asubuhi aliondoa maelezo na akabaki tu kuwa 'Mheshimiwa Raila Amolo Odinga'.

Haki miliki ya picha TWITTER

Wakenya mtandaoni waligundua hilo:

Sheria za Twitter huharamisha "kujionesha kuwa mtu mwingine kwa njia ya kukanganya au kuhadaa" na ukurasa kama huo unaweza kufungwa kabisa.

"Haufai kujifanya kuwa mtu mwingine, kundi au shirika kwa njia ambayo inanuiwa au inapotosha, kukanganya, au kuwahadaa wengine," zinasema sheria za Twitter.

Mada zinazohusiana