Mwanamke Japan aishtaki serikali kwa kumfunga kizazi kwa lazima

Nyenzo za upasuaji Haki miliki ya picha CARL DE SOUZA/AFP/GETTY IMAGES
Image caption Maelfu ya watu walifungwa vizazi nchini Japan bila idhini yao kwa sababu walionekana kuwa na kasoro za kiakili na kimwili

Mwanamke mmoja nchini Japan, ambaye alilazimishwa kufunga kizazi miaka ya 1970 akiwa na umri wa miaka 15, ameishitaki serikali katika kesi ya kwanza ya aina yake.

Mwanamke huyo ambaye hakutajwa jina lake ni mmoja wa wanawake 25,000 waliopitia upasuaji wa kuwafunga kizazi chini ya sheria ambayo kwa sasa haitekelezwi.

Waathiriwa walifungwa kizazi kwa sababu walibainika kuwa na magonjwa ya kiakili ama wenye matatizo kama vile ukoma.

Takriban 16,500 kati yao walidaiwa kufanyiwa upasuaji bila idhini yao.

Baadhi yao walikuwa wadogo wakiwa na umri hadi miaka tisa wakati huo.

Mwanamke huyo ambae kwa sasa ana umri wa miaka 60 na ushei, alichukua hatua ya kisheria baada ya kubaini kuwa alifungwa kizazi chake mwaka 1972 baada ya kupatikana na maradhi ''ya urithi ya kasoro ya ubongo".

Alikuwa na matatizo ya kiakili baada ya kufanyiwa upasuaji wa kumtengenisha na pacha wake waliyekuwa wameungana mwili alipokuwa mtoto mchanga, viliripoti vyombo vya habari vya Japan.

Kutokana na athari mbaya za kufungwa kizazi, baadaye alilazimika kuondolewa mfuko wa mayai ya uzazi (ovari).

Taarifa zinasema mwanamke huyo anataka alipwe fidia ya $101,000; kwa uharibifu huo aliotendewa kwenye mwili wake, akielezea kwamba haki zake kama binadamu zilikiukwa.

"Tulikuwa na siku za mfadhaiko wa kiakili... tulisimama kuifanya jamii hii iwe ya mwangaza," dada yake aliuambia mkutano wa waandishi wa habari.

Waziri wa Afya wa Japan Katsunobu Kato amekataa kutoa kauli yake kuhusiana na kesi hiyo, akisema kuwa hana maelezo yoyote kuhusiana nayo.

Afisa kutoka wizara ya afya aliliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali itakutana na kila mmoja wa waathiriwa waliofungwa uzazi wanaohitaji usaidizi, lakini "hakuna mipango wa kutoa fidia "kwa wote".

Sheria hiyo ambayo haitekelezwi ambayo ndiyo iliyotumika kuwafanyia upasuaji wa kufunga kizazi ilikuwepo baina ya mwaka 1948 hadi 1996.

Serikali za Ujerumani na Sweden, ambazo zilikuwa na sheria kama hiyo ya kudhibiti uzazi, ziliwaomba msamaha waathiriwa na kuwalipa fidia.