'Bomu' larushwa kwa naibu kiongozi wa upinzani Kenya Kalonzo Musyoka

Naibu wa muungano wa Nasa nchini Kenya Kalonzo Musyoka Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Naibu wa muungano wa Nasa nchini Kenya Kalonzo Musyoka

Maafisa wa kutegua mabomu katika nyumba ya kiongozi wa chama cha Wiper na naibu kinara mkuu wa muungano wa chama cha upinzani nchini Kenya- NASA, Bwana Stephen Kalonzo Musyoka, wanachunguza kifaa kinachofanana na bomu kilichorushwa katika nyumba yake mjini Karen, Nairobi.

Afisa mkuu wa polisi katika eneo la mtaa wa Karen Cunningham Suiyanka alisema kuwa kifaa hicho kinachofanana na guruneti kilirushwa katika nyumba ya Kalonzo Musyoka muda wa saa nane za usiku siku ya Jumatano.

Hakuna mtu aliyejeruhiwa kulingana na maafisa hao.

Walinzi wake wanasema kuwa watu wasiojulikana waliwasili katika eneo hilo na magari mawili wakafyatua risasi kabla ya kurusha kifaa hicho ndani ya eneo la makao hayo.

Siku ya Jumanne, Bw Musyoka hakushiriki katika hafla ya kuapishwa kwa kiongozi wa muungano wa Nasa Raila Odinga , hatua iliowakasirisha wanachama wengi wa mungano huo waliohudhuria.

Wakati alipotoka katika nyumba yake mjini Karen siku ya Jumanne alfajiri, kiongozi huyo wa Nasa hakutaka kutoa maelezo kuhusu mpango huo wa kuapishwa.

Huwezi kusikiliza tena
Mudavadi: Upinzani hauna nia ya kuzua vurugu Kenya

Bw Musyoka, ambaye awali alikuwa amesisitiza kuwa atakula kiapo hicho pamoja na kiongozi wa Nasa Raila Odinga, hakuonyesha imani ya kufanya hivyo .

''Sitaki kusema kuhusu mpango huo hivi sasa. Hatua ya Polisi kujiondoa hatujui. Lakini wafuasi wetu ni lazima wawe watulivu'', alisema katika mahojiano na waandishi ambao walikuwa wamepiga kambi nje ya nyumba yake.

Alikuwa akiandamana na sineta wa kituo hicho Enoch Wambua na Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana ambao hawakuzungumza na vyombo vya habari.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kalonzo, kushoto na Raila wakiwa katika mkutano wa muungano huo awali

Bwana Musyoka alisema kwamba yeye pamoja na viongozi wengine wa Nasa Moses Wetangula, Musalia Mudavadi na Raila Odinga watakutana kabla ya kuelekea Uhuru Park.

''Kwa kweli tutafanya majadiliano kuchunguza kiapo tunachokula na kutoa maelezo.Tutaambia taifa hatua tutakayoichukua'', alisema.

''Huu ni mpango muhimu wa harakati zetu kwahivyo tunajadiliana''.

''Vyombo vya habari vimefungiwa na lazima tuambie watu wetu kinachoendelea'', aliiongeza Musyoka.

Baadaye alifanya mkutano mwengine ambapo aliishutumu serikali kwa kuwapokonya walinzi viongozi wa Nasa.

Mada zinazohusiana