Marekani, EU na AU wamshutumu Odinga kwa 'kujiapisha' Kenya

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya akijiapisha kuwa ''Rais wa Wananchi'' Haki miliki ya picha EPA
Image caption Kiongozi wa upinzani nchini Kenya akijiapisha kuwa ''Rais wa Wananchi''

Serikali ya Marekaniimesema imesikitishwa na hatua ya kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ya kujiapisha Jumanne wiki hii.

Marekani pia imeishutumu serikali kwa kufungia vituo vinne vya habari nchini humo ambavyo viliadhibiwa baada ya kupeperusha moja kwa moja hafla hiyo ya upinzani.

Umoja wa Afrika na Muungano wa Ulaya pia wameshutumu hatua hiyo ya Bw Odinga.

Kupitia taarifa, wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema taifa hilo linaamini mizozo yoyote ile inafaa kutatuliwa kwa njia zifaazo kisheria.

"Tunakataa vitendo vyovyote ambavyo vinahujumu Katiba ya Kenya na utawala wa sheria. Uhuru Kenya alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya mnamo Oktoba 26, 2017 katika uchaguzi ambao uliidhinishwa na Mahakama ya Juu," taarifa hiyo iliyotumwa na msemaji wa wizara hiyo Hearther Nauerth imesema.

"Umoja wa Afrika unakataa vitendo vyote amabvyo vinahujumu mfumo wa kikatiba na utawala wa sheria. Mwenyekiti wa Tume (Moussa Faki Mahamat) anatoa wito kwawahusika wote kujiepusha na vitendo kama hivyo ambavyo pia vinatia hatarini uthabiti wa kisiasa Kenya," taarifa ya Tume ya Umoja wa Afrika imesema.

Bw Odinga, mgombea urais wa muungano wa National Super Alliance (NASA) uchaguzi wa tarehe 8 Agosti ambao matokeo yake yalibatilishwa baada ya kesi iliyowasilishwa naye Mahakama ya Juu, alisusia uchaguzi huo wa marudio na amesema hamtambui Rais Kenyatta kama rais halali wa taifa hilo.

Jumanne, alikula kiapo kuwa Rais wa Wananchi katika hafla iliyohudhuriwa na maelfu ya wafuasi wake uwanja wa Uhuru Park, Nairobi.

Mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka, ambaye ni makamu wa rais wa zamani, hakuhudhuria sherehe hiyo ingawa walikuwa wameahidi kuapishwa wote wawili kwa pamoja.

Image caption Wafuasi wa Bw Odinga wakisherehekea Kisumu baada yake kula kiapo Uhuru Park, Nairobi

Bw Musyoka baadaye alisema alipokonywa walinzi wake na hivyo kuzuiwa kuondoka nyumbani kwake kwenda kuhudhuria sherehe hiyo.

Bw Odinga alipokuwa anakula kiapo alisema Bw Musyoka angeapishwa baadaye.

Jumatano, mbunge wa upinzani Tom Joseph Kajwang' anayewakilisha eneo bunge la Ruaraka, Nairobi alikamatwa na akashtakiwa kwa makosa ya kuhudhuria mkutano haramu na kushiriki katika kulishwa kiapo kwa Bw Odinga kwa njia ya kudai kumfunga Bw Odinga "kutekeleza kosa la jinai la uhaini".

Bw Kajwang', ambaye ni wakili, alikuwa amevalia sare za uwakili na kwa pamoja na mshauri wa zamani wa Bw Odinga, Miguna Miguna, walikuwa karibu na Bw Odinga alipokuwa anakula kiapo.

Matukio makuu mzozo wa kisiasa Kenya

  • 8 Agosti, uchaguzi mkuu wafanyika ambapo Bw Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi
  • 1 Septemba, Mahakama ya Juu yabatilisha ushindi wa Bw Kenyatta katika kesi iliyowasilishwa na Bw Raila Odinga, na kuagiza uchaguzi urudiwe
  • 26 Oktoba, uchaguzi wa marudio wafanyika, huku upinzani ukisusia. Bw Kenyatta atangazwa mshindi.
  • 30 Januari, Bw Odinga ala kiapo kuwa 'Rais wa Wananchi' na kusisitiza kwamba hatambui Bw Kenyatta kama rais halali wa Kenya

Ijumaa, polisi walimkamata pia mshauri wa zamani wa Bw Odinga, Miguna Miguna, ambaye ndiye aliyetia saini hati ya kiapo cha Bw Odinga.

Kufungiwa kwa vituo vya habari

Marekani imesema imesikitishwa sana na vitendo vya serikali kwa "kufunga, kutisha na kuminya vyombo vya habari".

"Uhuru wa kujieleza, ikiwa ni pamoja na kwa wanahabari, ni muhimu sana kwa demokrasia, na umelindwa kwenye Katiba ya Kenya," taarifa ya Marekani imesema.

"Tunaihimiza serikali na Wakenya wote kuheshimu uhuru wa kujieleza na kutii agizo la mahakama na kuvifungulia vituo hivyo vya televisheni."

Mahakama ilikuwa imeamuru vituo hivyo vya Citizen, Inooro, NTV na KTN vifunguliwe Alhamisi lakini kufikia Ijumaa asubuhi, agizo hilo lilikuwa bado halijatekelezwa.

Ingawa Marekani imewasifu polisi na vikosi vya usalama kwa jinsi walivyosimamia hafla hiyo ya kuapishwa kwa Bw Odinga Jumanne, wamesema visa vya kukamatwa na kushtakiwa kwa washukiwa vinafaa kutekelezwa kwa kufuata sheria kikamilifu.

Marekani imewahimiza viongozi wa kisiasa Kenya kufanya mazungumzo kwa lengo la kuimarisha uwiano na utangamano na kutatua matatizo ya muda mrefu nchini humo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii