Mwanasiasa mkongwe Mzee Kingunge Ngombale Mwiru afariki dunia Tanzania

Magufuli Haki miliki ya picha IKULU, TANZANIA
Image caption Rais Magufuli alimjulia hali Mzee Kingunge alipolazwa hospitalini

Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania Kingunge Ngombale-Mwiru, 87, amefariki dunia, jamaa zake wameiambia BBC.

Mzee Kingunge amekuwa akitibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mwanasiasa huyo mkongwe alilazwa hospitalini mwanzoni mwa Januari akiuguza majeraha ya kushambuliwa na kung'atwa na mbwa nyumbani kwake 22 Desemba mwaka jana na akafanyiwa upasuaji.

Rais John Magufuli amesema apokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mzee Kingunge na kusema alikuwa mtu aliyechangia katika juhudi za kupigania uhuru wa Tanzania na na baada ya uhuru awaka mtumishi mtiifu wa chama cha Tanu na baadaye CCM.

"Ametoa mchango mkubwa sana, sisi kama taifa hatuwezi kusahau na tutayaenzi mema yote aliyoyafanya wakati wa utumishi wake uliotukuka," amesema Dkt Magufuli kupitia taarifa.

"Ametuachia somo la kupigania maslahi ya nchi wakati wote, kuwa wazalendo wa kweli, kudumisha Amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuwa na nidhamu."

Viongozi pia wametuma salamu zao za rambirambi na kumuomboleza mwanasiasa huyo akiwemo kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe.

Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki kutokaTanzania wanaomboleza kuondokewa na mwanasiasa huyo na kusema atakumbukwa kwa mchango wake katika maendeleo ya Afrika Mashariki.

"Ametoa mchango mkubwa na ni muumini wa uanajumuiya wa Afrika na siasa za ukanda. Ndugu Kingunge siku zote alisimamia muungano na umoja na alipinga sana utengano. Mzee Kingunge aliamini katika mshikamano na ushirikiano," wamesema kupitia taarifa.

Mzee Kingunge alikuwa mmoja wa viongozi wa muda mrefu na miongoni wa watu waliokuwa na ushawishi katika Chama cha Mapinduzi (CCM) hadi alipojiuzulu kutoka kwenye chama hicho Oktoba 2015 akilalamikia alichosema ni ukiukaji wa katiba ya chama hicho.

Kabla ya kujiuzulu, alikuwa amesema kwamba hakuwa amefurahishwa na utaratibu uliotumiwa kumteua mgombea urais wa CCM mjini Dodome Julai mwaka huo.

Hata hivyo, aliahidi kutohamia chama kingine.

Bw Kingunge alikuwa amehduumu katika CCM tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 1977.

Mke wake, Peras, alifariki dunia mwezi uliopita akitibiwa pia Muhimbili baada ya kulazwa kwa miezi kadha.

Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli alikuwa amefika katika Wodi ya Mwaisela iliyopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kumjulia hali Mzee Kingunge mwanzoni mwa mwezi Januari.

Wasifu wa Kingunge

Kingunge Ngombale Mwiru, mstaafu ambaye katika maisha yake toka ujana wake amelitumikia taifa mpaka hata ngazi za juu kabisa.

Alipata kushika nafasi mbalimbali nchini Tanzania zikiwamo mkuu wa Mkoa, mbunge na hata waziri kwa nyakati tofauti.

Historia yake inarudi nyuma kabisa katika kipindi cha nchi za Afrika zilipokuwa zikipigania kupata uhuru.

Kingunge alishiriki katika harakati akiwa mmoja wa vijana wa TANU walioshinikiza kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika.

Vyanzo kadhaa vinadai Kingunge ndiye aliyekabidhiwa jukumu la kuzigawa kadi mia za kwanza kabisa za wana TANU baada ya TANU kuanzishwa.

Kingunge alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwa na nafasi nyeti katika TANU na hata ilipokuja kuwa CCM mpaka pale alipoamua kuondoka CCM wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015 na kwenda upande wa upinzani akilalamikia alichosema ni ukiukaji wa katiba ya chama hicho kikongwe nchini Tanzania.

Kwa miaka yote Kingunge Ngombale Mwiru alikuwa mtu mwenye kusikilizwa na viongozi kama mshauri na pia mzoefu wa uongozi mwenye kuifahamu vizuri historia ya nchi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii