Raia wa Burundi wakatwa mishahara ili kuchangia hazina ya uchaguzi 2020

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza
Image caption Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza

Wafanyakazi wa umma nchini Burundi wameanza kukatwa mishahara ili kufadhili uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwaka wa elfu mbili na ishirini.

Katika kipindi cha miaka miwili ijayo, raia wote wa Burundi walio na zaidi ya umri wa kupiga kura wa miaka kumi na minane na zaidi, ni sharti wachangie katika hazina hiyo ya kitaifa.

Serikali ya Burundi imesema imechukua uamuzi huo ili kuziba pengo lililosababishwa na uamuzi wa wafadhili wa kuzuia misaada tangu mzozo wa mwaka wa elfu mbili na kumi na tano wakati rais Pierre Nkurunziza alipowania muhula wa tatu.

Hata hivyo serikali imekariri kuwa hazina hiyo ya uchaguzi ni wazo la raia wa Burundi wenyewe, pendekezo ambalo limepingwa na wakuu wa vyama vya wafanyakazi.

Huwezi kusikiliza tena
Tanzania yatahadharisha wahalifu waliotoka Burundi

Vyama hivyo havijafurahishwa na uamuzi huo wa kuwashurutisha raia kulipwa ushuru zaidi kufadhili uchaguzi na wamesema wanapanga kuwasilisha malalamishi yao kwa tume ya kitaifa ya majadiliano ili kutatua mzozo huo.

Awali vyama hivyo viliitisha mazungumzo na serikali kuhusiana na suala hilo na hadi sasa hilo halijatendeka.