Mnyarwanda wa kwanza kushiriki katika mashindano ya Tour de France

Areruya Joseph atakuwa mwendeshabasikeli wa kwanza kutoka Rwanda kushiriki shindano la Tour de France
Image caption Areruya Joseph atakuwa mwendeshabasikeli wa kwanza kutoka Rwanda kushiriki shindano la Tour de France

Mwendeshabaiskeli wa Rwanda akata tiketi ya kushiriki mashindano ya Tour de France kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo.

Nyota wa mbio za baiskeli wa Rwanda, Areruya Joseph ameshinda mashindano ya baiskeli ya Cameroon ambayo ni maalumu kwa waendeshabaiskeli waliochini ya umri wa miaka 23 barani Afrika.

Areruya Joseph mwenye umri wa miaka 21, alimshinda Chockri El Mehdi aliyechukua nafasi ya pili akiweka mwanya wa dakika 2 na sekunde 40.

Timu ya waendeshabaiskeli kutoka Rwanda pia ilishinda nafasi ya kwanza kati ya mataifa 13 ya Afrika yalishiriki mashindano hayo ikitangulia Morocco iliyoshika nafasi ya pili,huku Eritrea ikiambulia nafasi ya tatu.

Image caption Areruya Joseph ni mshindi wa mashindano ya baiskeli ya Cameroon

Ushindi huo wa Areruya Joseph umempa fursa ya kushiriki shindano kubwa ulimwenguni la Tour de France upande wa waliochini ya umri wa miaka 23,ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwa mwendeshabaiskeli kutoka Rwanda kushiriki shindano hilo.

Areruya Joseph ambaye anachezea timu ya Dimension Data ya Afrika ya Kusini, kwa sasa anashika nafasi ya tatu kwa viwango vya ubora barani Afrika.

Wiki iliyopita alishinda mbio za Gabon ambazo ni za kwanza barani Afrika.Wiki ijayo atakuwa miongoni mwa waendeshabaiskeli wa Afrika watakaoshiriki mashindano ya Afrika ya mbio za baiskeli kuwania ubingwa wa afrika ambayo yataandaliwa nchini Rwanda.

Mada zinazohusiana