Morgan Tsvangirai adaiwa kuwa hali mahututi

Waziri mkuu wa zamani nchini Zimbabwe na kiongozi wa chama cha upinzani MDC yuko katika hali mahututi
Image caption Waziri mkuu wa zamani nchini Zimbabwe na kiongozi wa chama cha upinzani MDC yuko katika hali mahututi

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai yuko hali mahututi katika hospitali moja nchini Afrika Kusini, kulingana na ripoti.

Vyombo vya habari viliinukuu vyanzo katika familia yake vilivyosema kuwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 65 ambaye anatibiwa saratani ya matumbo anakabiliwa na upungufu wa uzani , kuchoka na mishipa yake ya damu kua membamba.

Wakati wa harakati zake dhidi ya aliyekuwa rais wa Zimbabwe Robert Mugabe , amepigwa na kufungwa jela mara kadhaa.

Bwana Tsvangirai ndiye kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC nchini Zimbabwe.

Amekuwa akipelekwa hospitali mara kwa mara tangu mwezi Juni, akipokea tiba katika hospitali moja ya saratani mjini Johannesburg.

Alirejea hospitalini humo mwezi uliopita.

Afya ya bwana Tsvangirai ilidhoofika kwa haraka siku ya Jumatatu , kulingana na duru za familia zilizozungumza na mtandao wa Bulawayo24 siku ya Jumanne.

Alipoteza hamu ya kula na akawa na tatizo kubwa la kula ama hata kumeza maji, duru zilisema.

Bwana Tsvangirai pia ameripotiwa kuwa na tatizo la kupumua.

Wakati huohuo Duru za MDC zimesema kuwa bwana Tsvangirai yuko hali mahututi na kwamba watu wanafaa kutarajia lolote lile.

Msemaji wa Tsvangirai Luke Tamborinyoka alisema kuwa kiongozi huyo wa MDC yuko hali nzuri lakini taifa linafaa kumuombea.

Hospitali ambayo bwana Tsvangirai anatibiwa haijatoa tamko lolote kuhusu swala hilo.

Mada zinazohusiana