Kampuni ya ndege Nigeria yamlaumu abiria wake baada ya mlango kudondoka

A picture of the inside of the aircraft posted on Twitter by Dapo Sanwo. Haki miliki ya picha Twitter/@DapoSanwo
Image caption Abiria wanasema waliusikia mlango ukicheza wajati walikuwa angani katika safari ya kutoka Lagos hadi Abuja

Kampuni ya usafiri wa ndege imemlaumu abiria mmoja baada ya moja ya milango yake kudondoka punde tu walipotua.

Ndege hio iliosafiri kutoka Lagos hadi Abuja ilikuwa ikiambaa chini kwenye barabara ya kurukia ndege wakati mlango huo ulidondoka.

Kampuni hio ya Dana Air imekana kwamba chanzo cha tukio hilo lilikuwa la kiufundi na kusema mlango huo haungeweza kudondoka " bila jitihada za maksudi za abiria aliyeufungua"

Lakini abiria mmoja ameiambia BBC kuwa kila mmoja kwenye ndege alikataa kuuchokonoa mlango huo.

Dapo Sanwo kutoka Lagos alisema: "Safari nzima ilikuwa ya kelele na mitetemo kutoka sakafuni. Niliona kitasa cha mlango wa dharura kilikuwa kimelegea na kuning'inia."

"Tulipotua na ndege ikaanza kuambaa chini , tulisikia mlipuko mdogo, na wimbi kubwa la upepo na kelele. Ilikuwa mbaya sana."

"Wahudumu wa ndege walijaribu kumsingizia abiria kuwa alivuta kitasa lakini kila mmoja alikataa. Walijaribu pia kutuzuia kuchukua video na picha"

Katika taarifa iliotolewa na Dana Air, kampuni hio imekanusha kuwa na hitilafu yoyote katika safari nzima

"Milango yetu ya dharura imefungwa kikamilifu na hauwezi kudondoka bila mtu kuuchokonoa au kujaribu kwa maksudi kufunguliwa na mfanyakazi wa ndege au abiria," kampuni hio imesema.

" Wakati ndege inapokuwa angani, inakuwa katika mgandamizo wa juu na hamna njia ya kiti au mlango kutikisika kama inavyosemwa"

Kampuni iliendela kusema kuwa ndege ilikaguliwa na wahandisi pamoja na Mamlaka ya Usafirishaji wa Anga Nigeria na "hamna hitilafu iliyoripotiwa"

Mwaka 2012, ndege ya Dana Air ilianguka kwenye eneo la makazi jijini Lagos na kuwaua abiria 153.

Nigeria ina historia ya rekodi mbaya ya usalama wa anga. Mwaka jana , uwanja wa ndege wa Abuja ulifungwa kwa wiki sita kwa ajili ya marekebisho ya barabara ya kurukia ndege

Mada zinazohusiana