Dadake rais wa Korea Kaskazini awasili nchini Korea Kusini

Kim Yo-jong, dadake rais wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, amewasili nchini Korea Kusini
Maelezo ya picha,

Kim Yo-jong, dadake rais wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, amewasili nchini Korea Kusini.

Kim Yo-jong, dadake rais wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, amewasili nchini Korea Kusini.

Ni mtu wa karibu wa familia ya rais huyo kuzuru taifa hilo tangu vita vya Korea 1950-1953.

Yeye na Kim Yong Nam, kiongozi mwengine wa taifa la Korea Kaskazini wanaelekea Pyeongchang kuhudhuria ufunguzi wa mashindano ya Olimpiki ya msimu wa baridi.

Bi Kim ambaye anadaiwa kuwa na uhusiano wa karibu na nduguye alipandishwa cheo katika kamati kuu ya kisiasa nchini humo Politburo mwaka uliopita.

Maelezo ya picha,

Kiongozi wa Korea Kaskazini na rais wa marekani Donald Trump

Ni miongoni mwa watu waliowekewa vikwazo na Marekani kuhusiano na maswala ya ukiukaji wa haki za kibinaadamu.

Katika michezo hiyo ya Olimpiki mataifa yote mawili ya Korea kaskazini na Korea kusini yataingia katika sherehe ya ufunguzi wa michezo hiyo wakibeba bendera moja.

Mbali na wanariadha 22 Pyongyang pia itatuma zaidi ya wajumbe 400 katika michezo hiyo, ikiwemo kundi moja la mashabiki wake na bendi.

Diplomasia hiyo ya michezo inajiri wakati ambapo uhusiano kati ya mataifa hayo ya Korea umeimarishwa , ijapokuwa wataalam wametoa tahadhari kwamba hatua hiyo haijamaliza wasiwasi wa kieneo uliopo.

Rasi ya Korea imegawanyika tangu vita vya 1950-53 na pande hizo mbili hazijawahi kutia saini makubaliano ya amani .

Bi Kim anadaiwa kuwa na miaka 30 na ameshindwa na nduguye mkubwa kwa miaka minne.

Ziara yake inaonekana kuwa ishara kwamba Kim Jong un yuko tayari kuimarisha uhusiano na Korea Kusini, kulingana na mwandishi wa BBC wa maswala ya Korea Laura Bicker.

Baadhi wanadai kwamba huenda anawasilisha ujumbe kutoka kwa nduguye.