Chama cha ANC chaamua Zuma ni lazima aondoke

Muhula wa Zuma unamalizika mwaka ujao Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Muhula wa Zuma unamalizika mwaka ujao

Chama tawala Afrika kusini African National Congress (ANC) kimemuomba rasmi rais Jacob Zuma ajiuzulu baada ya yeye kukataa kufanya hivyo mapema hii leo, taarifa zinasema.

Taarifa kuhusu uamuzi huo umefuata mfululizo wa mazungumz ya maafisa wa juu wa chama hicho yalioendelea usiku kucha hadi kuamkia Jumanne alfajiri.

Iwapo Bwana Zuma, mwenye umri wa miaka 75, hatoteteleka, atakabiliwana kura ya kutokuwa na imani naye bungeni ambayo anatarajiwa kushindwa.

Akiwa amehudumu madarakani tangu 2009, ameandamwa kwa tuhuma za rushwa.

Chama cha ANC hakijathibitisha rasmi mipango yake lakini duru kutoka cham hicho zimetoa ufafanuzi katika vyombo vya habari nchini Afrika kusini na pia kwa shirika la habara la kimataifa la Reuters.

Rais Zuma amekiuka shinikizo linaloongezeka la kumtaka ajiuzulu tangu Desemba wakati Cyril Ramaphosa alipoichukua nafasi yake kama kiongozi wa chama cha ANC.

Katibu mkuu wa ANC Ace Magashule ameiwasilisha barua kwa kiongozi huyo anayepigwa vita nyumbani kwake katika mji mkuu Pretoria, na kumuarifu rasmi kuhusu uamuzi wa chama hicho wa kumtaka aondoke katika mkutano na kamati ya kitaifa ya utendaji (NEC), taarifa zinasema.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Imebainika kuwa mrithi wake Zuma atakuwa Cyril Ramaphosa kwasababu ndiye rais wa chama cha ANC.

Kimsingi rais Zuma amekubali kuondoka lakini anataka muda wa ilani wa kati ya miezi 3 na 6.

Hakujatolewa muda wa mwisho kwake kuondoka madarakani, lakini imebainika kuwa mrithi wake atakuwa Cyril Ramaphosa kwasababu ndiye rais wa chama cha ANC.

Hatua hii ya ANC inaonekana ndio njia rahisi zaidi ya chama hicho kumng'oa rais Zuma madarakani badala ya kusubiri utaratibu wa bunge ambao ungeweza kuwa mrefu na wenye madhara zaidi kwa chama cha ANC.

Rais Jacob Zuma ambaye anakabiliwa na mashtaka kadhaa ya rushwa, alishindwa uongozi wa chama tawala Desemba mwaka jana.

Kiongozi mpya wa ANC, Cyril Ramaphosa anaongoza shinikizo za kumuondoa Zuma katika nafasi yake hiyo ya Urais, na hatimaye kushika pia nafasi hiyo.

Ramaphosa ameahidi pia kupambana na rushwa iliyokithiri na kukijenga upya chama cha ANC, wakati nchi hiyo ikielekea katika uchaguzi mwakani.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii