Wapinzani waendelea na mgomo Ethiopia

Waandamanaji nchini Ethiopia Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waandamanaji nchini Ethiopia

Waandamanaji wanaoipinga serikali katika mkoa ulio mkubwa nchini Ethiopia wa Oromia wanafanya mgomo wa siku tatu kushinikiza madai yao ya kuachiwa kwa wanasiasa wote na Waandsihi wanaoshikiliwa katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili kilichotokea machafuko.

Katika siku ya kwanza ya mgomo huo, jana Jumatatu, barabara nyingi ziliwekewa vizuizi na biashara kufungwa.

Hata hivyo serikali ya Ethiopia imesema itamwachilia huru kiongozi mgonjwa wa upinzani, licha ya maandamano kuendelea katika baadhi ya maeneo ya nchi.

Mwendesha mashtaka mkuu nchini Ethiopia ametangaza kuwa serikali itamuondolea mashtaka ya kuchochea ghasia Katibu Mkuu wa chama cha Oromo Federalist Congress.

Kiongozi huyo wa upinzani alikamatwa Desemba, 2015 kwa mashtaka ya awali ya kuwa na mahusiano na vikundi ya kigaidi. Lakini hata hivyo mashtaka hayo baadaye yalishushwa na kubadilika kuwa uchochezi wa ghasia.

Ataachiwa huru pamoja na wenziye sita aliokamatwa nao.

Serikali pia imewaachia huru na kuwaondolea mashtaka maelfu ya watu, ikiwa sehemu ya mageuzi iliyoahidi kumaliza maandamano ya upinzani yaliyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu nchini humo.

Mwaka 2016 hali ya hatari ilitangazwa na maelfu ya waandamanaji walikamatwa.

Mada zinazohusiana