Mwanasheria mkuu wa Kenya Profesa Githu Muigai ajiuzulu

Mwanasheria mkuu wa Kenya Professa Githu Muigai Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mwanasheria mkuu wa Kenya Professa Githu Muigai

Mwanasheria mkuu wa Kenya Profesa Githu Muigai amejiuzulu baada ya kuhudumu kwa miaka sita na nusu.

Rais Uhuru Kenyatta amemshukuru Profesa Githu kwa huduma zake na sasa jaji Paul Kihara Kariuki atachukua mahala pake.

Haki miliki ya picha Twitter
Image caption Ujumbe wa rais Uhuru Kenyatta aktika mtandao wa Twitter

''Nimepokea kwa majuto uamuzi wa mwanasheria mkuu Githu Muigai . Namshukuru kwa huduma yake katika kipindi cha miaka sita na nusu. Nimemteua jaji Paul Kiharara Kariuk''i , Rais Uhuru Kenyatta alichapisha katika mtandao wake wa Twitter.

Kabla ya uteuzi wake kuwa mwanasheria mkuu profesa Muigai alikuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni ya mawakili ya Mohammed Muigai na amekuwa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na ubaguzi wa rangi.

Alikuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha sheria cha Columbia mjini New York . Kutoka 1984 alikuwa mwanfunzi katika chuo cha kusomea uanasheria nchini Kenya .

Vilevile alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi .

Akiwa mshauri wa serikali katika maswala ya kisheria, Githu Muiga atakumbukwa kwa kuleta sheria za mageuzi katika timu ya uchaguzi nchini Kenya siku chache tu kabla ya uchaguzi kufanyika.

Katika sheria hiyo kamishna yeyote yule katika tume ya uchaguzi alipewa nguvu za kumtangaza mshindi wa uchaguzi iwapo mwenyekiti wa tume hiyo hayupo.

Sheria hiyo ilizua pingamizi kutoka kwa upinzani pamoja na jamii ya kitaifa waliodai kuwa serikali haiwezi kufanya mabadiliko ya sheria za uchaguzi wakati ambapo uchaguzi mkuu unakaribia.

Vilevile Githu Muigai atakumbukwa na hatua ya kuliharamisha kundi la upinzani la NRM hatua ambayo pia ilipingwa na viongozi wa upinzani wakisema kuwa ni hatua mojawapo ya serikali ya kutaka kukandamiza upinzani.

Siku chache kabla ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kula kiapo cha kuwa 'rais wa wananchi' , Bwana Githu alitishia kuwa mtu atakayejaribu kula kipao cha urais atajilaumu mwenyewe kwa kuwa mashtaka yatakayomkabili ni ya uhaini ambao hukumu yake ni mtu kunyongwa.

Hatahivyo Raila alikula kiapo hicho katika bustani ya Uhuru Park katika hafla iliohudhuriwa na maelfu ya wafuasi wa upinzani. Matokeo yake yalisababisha viongozi wa karibu walioshiriki katika kumlisha bwana Raila Kiapo hicho kukamatwa na kushatkiwa huku wengine wakifurushwa kutoka nchini.

Hatahivyo viongozi wengine wakuu wa upinzani hawakuhudhuria hafla hiyo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii