Rais Jacob Zuma: Sijafanya makosa yoyote na sioni sababu ya kujiuzulu

Rais Jacob Zuma wa Afrika ya kusini amesema kuwa haoni sababu ya yeye kujiuzulu
Image caption Rais Jacob Zuma wa Afrika ya kusini amesema kuwa haoni sababu ya yeye kujiuzulu

Rais wa Afrika kusini Jacob Zuma anasema hajafanya makosa na haoni sababu ya kujiuzulu.

Bwana Zuma alizungumza baada ya chama tawala cha ANC kumpatia makataa ya kujiuzulu mwisho wa siku la sivyo akabiliwe na kura isiokuwa na imani dhidi yake siku ya Alhamisi.

Rais huyo amekuwa chini ya shinikizo ya kujiuzulu huku kukiwa na madai mengi ya ufisadi.

Lakini amesema kuwa ANC imeshindwa kuelezea ni kwa nini ametakiwa kujiuzulu.

''Haijakuwa haki kwangu mimi kwamba tatizo hili limeangaziwa'', aliambia kituo cha habari cha SABC wakati wa mahojiano marefu ambayo hayakuwa yametangazwa rasmi.

''Hakuna mtu aliyetoa sababu .Hakuna mtu anayesema kilichofanyika'', Alisisitiza kwamba hakipuuzi chama cha ANC lakini amekataa kukubaliana na uamuzi wa kumtaka kujiuzulu.

Bwana Zuma amesema kuwa yuko tayari kuondoka baada ya mwezi Juni , lakini akapinga vile jambo hilo linavyoangaziwa kwa sasa .Alisema kwamba atatoa taarifa nyengine baadaye siku ya Jumatano.

Chama cha ANC kimesema kuwa kilisikiza matamshi ya Bwana Zuma lakini kitatoa uamuzi wa hatua yake baadaye kabla ya kuzungumza.

Awali kiranja wa chama hicho Jackson Mthembu alitangaza kwamba kura isiokuwa na imani dhidi ya rais itasikizwa siku ya Alhamisi huku Cyril Ramaphosa aliyechaguliwa kuwa rais wa chama hicho mwezi Disemba akiapishwa mara moja kuwa rais wa taifa hilo.

Mkutano wa kamati kuu ya ANC ulikuwa umetangaza uamuzi wake wa kumtaka Zuma ajiuzulu siku ya Jumanne na kumpatia hadi mwisho wa siku siku ya Jumatano kujiuzulu.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Familia ya Gupta imetuhumiwa kwa kutumia uhusiano wa karibu na rais kuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa.
Haki miliki ya picha SOUTH AFRICAN PRESIDENCY
Image caption Atul Gupta akisalimiana na rais Zuma

Katika mahojiano , bwana Zuma hakuzungumza kuhusu uvamizi wa mapema alfajiri uliotekelezwa na maafisa wa polisi katika nyumba ya washirika wake wakuu familia ya Gupta siku ya Jumatano.

Familia ya Gupta imetuhumiwa kwa kutumia uhusiano wa karibu na rais kuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa.

Pande zote mbili zimekataa kuwepo kwa madai hayo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii