Tanzania kutaifisha meli ya uvuvi ya China

Moja kati ya meli zilizorejea bandari ya Tanzania kwa ajili ya ukaguzi
Maelezo ya picha,

Moja kati ya meli zilizorejea bandari ya Tanzania kwa ajili ya ukaguzi

Serikali ya Tanzania imeliamuru jeshi la polisi na mamlaka ya uvuvi wa bahari kuu nchini humo kupeleka ombi mahakamani kuomba kibali cha kuitaifisha meli ya China iliyokamatwa katika eneo lake ndani ya bahari ya hindi ikifanya uvuvi usiokubalika na uchafuzi wa mazingira.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina meli hiyo ilikamatwa mwishoni mwa mwezi Januari.

Baada ya kukaguliwa ilikutwa na mikia na mapezi ya papa jambo ambalo haliruhusiwi kwa mujibu wa sheria za uvuvi wa bahari kuu kuvua papa na kukata sehemu hizo muhimu na kumtupa baharini jambo ambalo pia ni uchafuzi wa mazingira.

Meli hiyo ya Buhanaga 1 kutoka nchini China iliamuriwa kulipa faini ya dola za kimarekani laki tatu na nusu $350,000, ndani ya siku saba jambo ambalo halija tekelezwa na wamiliki wa meli hiyo tayari zimepita takribani siku 20.

Maelezo ya picha,

Samaki waliokaguliwa wakihifadhiwa kwenye barafu

Serikali ya Tanzania imesema haiwezi kutoa muda zaidi badala yake imeelekeza taratibu zifanyike kuiomba mahakama waitaifishe pamoja na tani 42 za samaki, mikia na mapezi ya papa pamoja na tani nne za samaki ambao wako chini ya kiwango.

Kwa mujibu wa sheria za uvuvi za Tanzania na zile uvuvi za bahari kuu, Tanzania imetoa vibali vya uvuvi wa bahari kuu kwa meli 24.

Kabla ya kupatiwa leseni zilikaguliwa na kudhinishwa kufanya uvuvi ndani ya bahari kuu kwa maelekezo baada ya kumaliza kuvua ni lazima zirejee kwa ukaguzi kabla ya kuondoka lakini kati ya hizo ni nane pekee zimerejea kwa ajili ya ukazi na 16 zilizosalia zimetoroka na Waziri mwenye dhamana ameelekeza zitafutwe na hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria za uvuvi za Tanzania na za kimataifa