Waziri mkuu wa Ethiopia ajiuzulu

Waziri mkuu nchini Ethiopia Hailemariam Desalegn
Image caption Waziri mkuu nchini Ethiopia Hailemariam Desalegn

Waziri mkuu nchini Ethiopia Hailemariam Desalegn amejiuzulu .

Imedaiwa kuwa kiongozi huyo aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa chama chake cha Ethiopia People's Demecratic front.

Hatahivyo haijabainika iwapo chama hicho kimekubali uamuzi wake au la.

Hailemariam Desalegn amesema kuwa amejiuzulu ili kusaidia kusuluhisha mzozo wa kisiasa uliopo nchini humo.

Katika hotuba aliyotoa kwenye televisheni ya taifa kiongozi huyo amesema, ''Chama tawala cha Ethiopia Peoples Revolutionary Democratic Front na serikali inataka kupata ufanisi wa mabadiliko yaliowekwa katika wakati ambapo kuna mgogoro na matatizo ya kisiasa nchini ambapo watu wengi wamepoteza maisha yao, wengine makao huku mali zao zikiharibiwa na kuna juhudi za kuharibu uwekezaji uliopo.

'Ili kupata suluhu na ufanisi wa mabadiliko yaliowekwa, na suluhu tulioweka nimewasilisha barua ya kujizulu majukumu yangu katika serikali na katika chama kwa hiari yangu', alisema katika hotuba iliopeperushwa katika runinga ya taifa EBCTV.

Kuondoka kwake kunatokea wakati ambapo kumeshuhudiwa maandamano ya miezi dhidi ya serikali katika maeneo makuu nchini humo Oromia na Amhara.

Katika ghasia za mwisho zilizoshuhudiwa, watu 10 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika maandamano ya upinzani.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ethiopia imekumbwa na maandamano ya zaidi ya miaka miwili ya kuipinga serikali, mara nyingi yanayoongozwa na jamii ya Oromo

Mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza, aliyepo katika mji mkuu Addis Ababa, anasema serikali imewaachia huru maelfu ya wafuasi wa upinzani kutoka gerezani na waandishi habari katika wiki za hivi karibuni, lakini bado maandamano hayo yameendelea kushuhudiwa.

Ethiopia imeshuhudia maandamano mengi yaliokumbwa na ghasia tangu mnamo 2015, huku waandamanaji wakiitisha mageuzi ya kisiasa na kiuchumi na kutaka rushwa isitishwe serikalini.

Ghasia hizo zinazoendelea zimesababisha mgawanyiko mkubwa katika serikali ya muugano, anasema mhariri wa BBC wa masuala ya Afrika.

Miongoni mwa matajiri wa Ethiopia wanamuona waziri mkuu huyo kama mdhaifu na aliyekosa muelekeo, ameongeza.

Ethiopia ikigeuka kuwa nchi dhaifu na inayokumbwa na misuko suko ni hatari kwa eneo zima la Pembezoni mwa Afrika, anaongeza mwandishi wetu - kwasababu taifa hili ambalo kwa kawaida lina utulivu linaonekana kama msingi wa kulishikanisha eneo zima pamoja.

Muungano tawala wa vyama vinne upo katika mkutano wa dharura hivi sasa. Hatua hiyo ya kujiuzulu kwa waziri mkuu Desalegn itahitajika kuidhinishwa na bunge la Ethiopia.

Bwana Hailemariam aliingia madarakani mnamo Agosti 2012, baada ya kufariki kwa kiongozi shupavu Meles Zenawi.

Katika uchaguzi wa 2015, muungano wake ulijinyakulia viti vyote bungeni.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii