Mahandaki na watawala wa Afrika

  • Rashid Chilumba
  • Mchambuzi wa maswala ya siasa
Trump - akisimama mbele ya nyumba yake ya Mar-a-Lago

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Trump ana handaki ndani ya nyumba yake ya Mar-a-Lago estate - lakini halina uhusiano wowote na yeye kuwa rais

Vita kuu vya dunia, vita baridi na wasiwasi wa miaka ya karibuni kuhusu mataifa kushambuliana kwa nyuklia kumezifanya serikali nyingi duniani kuwekeza zaidi kwenye ulinzi wa viongozi wake kwa kufadhili miradi mikubwa ya ujenzi wa mahandaki ya kisasa na maeneo zaidi ya maficho ili kuwanusuru watawala ikiwa dharura itatokea.

Mathalan, karne ya 21 imetawaliwa na kitisho cha mashambulizi ya nuklia na hivyo mataifa karibu yote makubwa yakiongozwa na Marekani yamewekeza katika miundombinu, hasa ujenzi wa mahandaki na maeneo ya maficho yenye uwezo wa kutoa makaazi ya muda kwa rais na viongozi waandamizi wa serikali ikiwa shambulio litatokea.

Mzozo baina ya marekani na Korea Kaskazini juu ya mpango wa nyuklia wa taifa hilo la Bara Asia ulifichua mengi, ikiwemo maswali ya ni wapi rais wa Marekani na wasaidizi wake wakuu watajificha iwapo vita vya nuklia vingezuka.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

handaki la Greenbrier, ambalo lilikuwa likitumiwa Congress, sasa ni kivutio cha utalii

Maswali hayo yameibua mjadala mpana kuhusu mataifa makubwa lakini vipi kuhusu Afrika?

Viongozi wake wanayo maeneo ya maficho kama mahandaki ya kisasa na njia za chini kwa chini kuwaepusha na balaa lolote likitokea?

Yamkini Bara la Afrika halimo sana kwenye ramani ya mjadala huo lakini viongozi wake hawapo nyuma kwenye kuimarisha mifumo ya kujilinda japo inaonekana kumekuwa na siri na kificho kikubwa juu ya mifumo ya maficho barani humo kuliko katika mataifa mengine duniani.

Pengine, tofauti kubwa baina ya viongozi wa Afrika na wale wa mataifa kama Marekani juu ya kutengeneza mahandaki na maeneo ya maficho ni tofauti.

Watawala wa Afrika wanahofia vitu kama mapinduzi ya kijeshi yasiyotarajiwa au machafuko yanayoweza kuyafikia maeneo yao ya makazi.

Matukio machache yaliyowatokea viongozi wa Afrika yalifichua siri nzito kuhusu uwepo wa maeneo ya maficho hasa mahandaki.

Ghadaffi na mahandaki lukuki

Wakati wa mapigano na waasi yaliyoangusha utawala wake, Muamar Ghadafi inasemekana alitumia mahandaki yaliyojengwa karibu na eneo lake la makazi kama sehemu ya maficho.

Hayo yalibainika baada ya utawala wake kuangushwa.

Chanzo cha picha, Mark Renders

Maelezo ya picha,

Muammar Gaddafi

Eneo maarufu zaidi ikiwa ni hekalu la Bab Al Aziziya lililopo katikati mwa jiji la Tripoli.

Bab Al Aziziya ndio ilikuwa makazi ya Ghadafi. Chini ya majumba ya kifahari ya Al-Aziziya kulikuwa na handaki kubwa la kisasa, inasemakana lilikuwa na njia za chini kwa chini hadi uwanja wa ndege wa Tripoli hivyo ingeweza kutumika kumtorosha Ghadafi na familia yake bila kugundulika.

Mahandaki kama hayo pia yaligunduliwa mjini Benghazi na mji wa nyumbani kwa Ghadafi wa sirte.

Mengi ya mahandaki hayo yaliyosanifiwa na kujengwa na makampuni ya kiswisi na kimarekani baina ya miaka ya 1970-1980.

Chanzo cha picha, ROBERTO SCHMIDT

Maelezo ya picha,

.

Ripoti za vituo vya habari zilionesha kuwa mahandaki hayo yalikuwa na hifadhi ya maji na chakula cha kutumiwa majuma kadhaa, jiko, vyumba vya kulala na mifumo ya mawasiliano, majenereta kwa ajili ya dharura ya ukosefu wa nishati na viyoyozi kukiwa na mifumo ya kuchuja hewa inayoweza kuzuia madhara ya silaha za sumu na athari za bomu la nyuklia pamoja na vyumba vya upasuaji na hospitali ndogo.

Gbagbo na handaki lake ndani ya Ikulu

Mwaka 2011 mwanasiasa mkorofi wa Code de'vote Laurent Gbagbo aliyekataa kukabidhi madaraka kwa mshindi wa uchaguzi wa 2010 Allasaine Outara.

Gbagbo alikamatwa na kikosi cha jeshi akiwa amejificha kwenye handaki lililojengwa chini ya makazi yake akiwa na mkewe na mwanawe wa kiume.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Bw Gbagbo na mke wake Simone walipelekwa kwenye chumba cha hoteli baada ya kukamatwa Aprili 11, 2011

Kikosi hicho tiifu kwa rais mteule Allasaine Ouatara kilifanya kazi ya ziada kulifikia eneo hilo katika wakati ambao Gbagbo aligoma kusalimu amri.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Vikosi vya Umoja wa taifa vilisaidia wanajeshi waliomuunga mkono Ouattara kumtoa Bw Gbagbo madarakani

Inaaminika watawala wengi wa nchi za Afrika ya kati na zile za Magharibi mwaka Afrika kama Guinea Equator, Gabon, Gogo, Cameroon, Gambia na Chad wanamiliki mahandaki ya kisasa yaliyo tayari kuwapa hifadhi mambo yakienda kombo, tishio kubwa ikiwa ni kutolewa madarakani kwa njia ya mapinduzi au maandamano ya umma.

Mobutu Sese Seko na rekodi ya handaki la kudhibiti mionzi ya nyuklia

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Mobutu Sese Seko aliitawala Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliyokuwa Zaire, kwa miaka 30

Mobutu Sese Seko, mtawala wa DR Congo zamani Zaire aliyejipatia ukwasi kwa kufisidi mali za taifa lake isingetarajiwa aishi bila ya mifumo ya ulinzi kama handiki.

Licha ya taarifa kudai alijenga mahandaki mengi nchini Zaire, lakini lililo maarufu zaidi ni lile la mjini Gbadolite, mji uliopo maili 710 Kaskasizi Mashariki mwa Kinshasa.

Handaki hilo kwa wakati huo ndiyo pekee katika Afrika ya Kati lilikuwa na uwezo wa kuzuia athari za shambulio la nuklia.

Pia lilikuwa na uwezo wa wa kuhifadhi watu 500 na ilikuwa limeunganishwa kuelekea Mto Ubangui kwa njia ya chini kwa chini ikitoa nafasi ya kuifikia bandari ya kijeshi katika kijiji cha N'dangi na hivyo kuwa rahisi kwa Mobutu kutoroka bila kukamatwa au kupata athari.

Viongozi wa upinzani je?

Katika tukio la kushangaza imethibitika sio walio mamlakani pekee ndiyo huwekeza kwenye ujenzi wa maeneo rasmi ya maficho.

Mwaka 2017 maafisa kadhaa wa polisi walifunguliwa mashatka ya kutaka kumuua kiongozi wa upinzani nchini Zambia Hakainde Hichilema baada ya kumpulizia kwa wingi gesi ya kutoa machozi ili kumlazimisha kutoka katika maficho ndani ya handaki lililo kwenye makazi yake mjini Lukasa, nchini Zambia.

Maafisa hao wa polisi walijitetea kuwa hapakuwa na njia nyingine ya kuchukua kwa sababu wasingeweza kuingia ndani ya handaki hilo.

Afrika Mashariki je?

Hakuna rekodi kamili juu ya kuwepo mifumo ya ulinzi na maficho ya chini kwa chini katika ikulu au makazi ya marais katika nchi za Afrika Mashariki, lakini inaaminika itakuwa imeundwa.

Nchi kama Uganda ambayo iliongozwa na viongozi waliopita jeshini kama Idd Amin na sasa Yoweri Museveni au Rwanda ya rais Paul Kagame mahandaki na maficho ni njia muhimu kujikinga dhidi ya adui hivyo kwa vyovyote lazima mifumo ya aina hiyo itakuwepo.

Kwa kuwa mifano yote ya mifumo hiyo kuthibitika ni hadi pale kitisho kinapotokea huenda siku mambo yakichacha kwa watawala wa maeneo hayo, siri zitafichuka juu ya uwepo wa mahandaki na maeneo yao ya maficho.

Inalinda?

Kwa bahati mbaya historia kwa Barani Afrika inaonesha mifumo hiyo ya ulinzi na maficho haijasaidia sana. Ghadafi, Gbagbo au Mobutu waliishia kutolewa madarakani licha ya kuwa na mahandaki.