Kisa cha kwanza cha mwanamume aliyejibadilisha jinsia 'kumnyonyesha mtoto'

Mtoto ananyonya

Chanzo cha picha, Getty Images

Mwanamume aliyejibadilisha jinsia na kuwa mwanamke amefanikiwa kumyonyesha mtoto katika kisa cha kwanza cha aina yake kuwahi kushuhudiwa, watafiti wanasema.

Mwanaume huyo ambaye sasa ni mwanamke mwenye umri wa miaka 30 alitaka kumnyonyesha mtoto baada ya mpenzi wake aliyejifungua kusema hataki kumnyonyesha mtoto huyo, hayo ni kwa mujibu wa jarida la afya la watu waliojibadili jinsia.

Alifanikiwa kunyonyesha baada ya kumeza dawa na kukamua maziwa, ripoti hiyo inasema kutoka nchini Marekani.

Mtaalamu wa Marekani anasema utafiti huo huenda ukachangia visa zaidi vya wanaume kujibadilisha jinsia na kuwa wanawake kunyonyesha watoto.

Mwanamke huyo aliyekuwa anapokea matibabu ya kubadili homoni zake mwilini kwa muda wa miaka 6, lakini hajafanyiwa upasuaji kubadili sehemu zake za siri, wakati alipowaomba madaktari wamsaidie atimize lengo lake la kumnyonyesha mtoto.

Kabla ya mtoto huyo kuzaliwa, madakatari walimpa dawa za miezi mitatu unusu kumsaidia kupata maziwa, kwa kawaida dawa hizo hupewa wanawake waliowaasili watoto au waliojipatia watoto kupitia wanawake wanaobeba mimba kibiashara kuwaisaidia wasioweza kuzaa.

Dawa hizo husisimua homoni mwilini kushinikiza kutoa maziwa na kuzuia homoni za kiume na pia alihitajika kukamua maziwa yake.

Na matokeo yake, yalimsababisha mwanamke huyo kuweza kupata maziwa kiasi.

Watafiti wanasema mtoto huyo alikunywa maziwa hayo tuu kwa wiki zake sita za uhai, wakati ambapo ukuwaji wake, ulaji na uwendaji haja wake ulikuwa unaendelea kama kawaida.

Baada ya hapa, mtoto alianza kupewa maziwa ya mkebe kwasababu maziwa yalianza kupungua.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Watafiti wamesema utafiti zaidi unahitajika kubaini matibabu halisi ya wanaume wanaojibadili jinsia kuwa wanawake wanaotaka kunyonyesha

Dkt Channa Jayasena, mhadhiri mkuu katika chuo cha Imperial College anayejishughulisha na masuala ya uzazi amesema, utafiti huo ni 'hatua nzuri'.

Amesema ameshasikia visa kadhaa nchini Uingereza vya wanaume waliogeuka kuwa wanawake wanasaidiwa kunyonyesha, lakini mpaka sasa hakuna ripoti iliyochapishwa.

Amesema:"Tunachohiaji kufanya nikuvikusanya visa hivi na tusaidiane kimawazo, tutafute mbinu muafaka kuwasaidia kunyonyesha bila ya kuwadhuru ki afya."

Watafiti wanasema haijabainika wazi iwapo dawa zote zinazotumika zinahitajika kufanikisha wazazi hao kuwawezesha kunyonyesha.

Wamesema uchunguzi zaidi unahitajika kubaini matibabu halisi ya wanaume wanaojibadili jinsia kuwa wanawake wanaotaka kunyonyesha.