Mkewe Aboud Rogo ahukumiwa miaka 10 Kenya kwa kupanga shambulio

Hania Rogo na wakili wake Aboubakar Yusuf kortini 2016
Maelezo ya picha,

Hania Rogo na wakili wake Aboubakar Yusuf kortini 2016

Mahakama moja nchini Kenya imemhukumu mwamamke mmoja kifungo cha miaka kumi kwa kosa la kupanga njama ya kufanya shambulizi la kigaidi.

Mahakama imempata na hatia Haniya Said Saggar ya kuratibu shambulio la bomu la petroli lililotekelezwa dhidi ya kituo cha polisi jijini Mombasa miaka miwili iliyopita. Haniya ni mjane wake Aboud Rogo, ambaye aliaminika kuandaa shughuli za kundi la wanamgambo wa Al Shabaab nchini Kenya.

Kwenye hukumu yake, hakimu alisema kulikuwa na ushahidi wa kutosha kwamba Haniya aliwasiliana na mmoja wa wanawake watatu waliolitekeleza shambulio hilo.

Mwanamke huyo, Tasnim Yakub, alikuwa amesilimu kutoka Ukristo miezi mitatu kabla ya shambulio, ikiwa ndio muda pia ambao alipata kujuana na Haniya.

Aboud Rogo

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Aboud Rogo

Mahakama imefahamishwa pia kwamba wawili hao waliendelea kuwasiliana hadi muda mfupi kabla ya shambulio hilo.

Inadhaniwa pia kwamba Tasnim aliwavutia wanawake wawili aliojiunga nao kukiteketeza moto kituo cha polisi na hata kujaribu kumdunga kisu askari. Wote watatu walipigwa risasi na kuuawa.

Ripoti ya ushahidi uliotokana na uchunguzi umebaini kwamba kipakatilishi cha Tasnim kilikuwa na fasihi zenye itikadi kali baadi ambazo zilichapishwa na kiongozi wa kidini mweye misimamo mikali Aboud Rogo - marehemu mumewe mshtakiwa.

Sheikh Rogo aliunga mkono wazi wazi kundi la Al Shabaab na pia alitetea mauaji ya wakristo.

Haniya Rogo
Maelezo ya picha,

Haniya Rogo

Rogo mwenyewe aliuawa kwa kupigwa risasi mara kumi na sita na watu wasiojulikana mnamo mwaka 2012 , tukio ambalo lilizua maandamano na tafrani jijini Mombasa.

Rogo aliaminika kuwa na uhusiano wa karibu na raia wa Uingereza Samantha Lethwaite, al Maarufu 'white widow', anayetuhumiwa kufadhili mauaji nchini Kenya, na ambaye angali anasakwa vikali na Polisi wa kimataifa, Interpol.