Mauaji ya Florida: Donald Trump aishutumu FBI

Shambulio la bunduki siku ya Jumatano huko Parkland, lilikuwa baya zaidi nchini Marekani tangu shambulio la 2012 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Shambulio la bunduki siku ya Jumatano huko Parkland, lilikuwa baya zaidi nchini Marekani tangu shambulio la 2012

Rais wa Marekani Donald Trump, ameirushia cheche za maneno shirika la upelelezi nchini humo- FBI, kwa kukosa kupata vidokezi muhimu vya mapema, kuhusiana na shambulio la Jumatano huko Florida, wakati mtu mwenye silaha alipowashambulia wanafunzi wa shule na kuwauwa watu 17.

Amesema kuwa FBI inapoteza muda mwingi kujaribu kubaini kuwa timu yake ya Kampeini ya Urais ilishirikiana na Urusi kuiba kura mwaka 2016 badala ya kutoa uilinzi kwa wamarekani.

Katika mtandao wake wa Tweeter, Bwana Trump, ameandika kuwa FBI inafaa kuzingatia kazi yake muhimu, huku akiongeza kusema kuwa, ni huzuni kubwa na ni jambo lisilokubalika kwamba, dalili ya uwezekani wa kutokea mashambulizi, haikutambuliwa mapema.

Awali Maelfu ya watu huko Florida, wakiwemo manusura wa kisa hicho cha Jumatano walijumuika pamoja katika mkutano mkubwa, wakitoa wito wa kuwepo kwa sheria ya udhibiti silaha nchini Marekani.

Aidha Bwana Trump amelaani kitendo hicho kiovu kilichotekelezwa na mvulana Nikolas Cruz.

Image caption Waandamanaji wakibeba mabango wakitaka sheria za kudhibiti silaha ziwekwe

Mkutano huo umefanyika nje ya mahakama ya jimbo hilo katika mji wa Fort Lauderdale, kilomita chache kutoka kwenye shule ambayo mwanafunzi wa zamani, Nikolas Cruz, aliwauwa watu 17.

Waandamanaji walibeba mabango yenye maandishi, 'Enough is Enough!' "imewtosha Kabisa" huku wakipaza sauti "No More Guns!" yaani "hakuna Bunduki tena!"

Tumekuwa na ukosoaji mkubwa dhidi ya Rais Donald Trump, ambaye kufikia sasa amekataa katu, kutoa nafasi kwa sheria kali ya kudhibiti silaha nchini Marekani.

Ametaja kisa hicho cha ufuatuaji risasi, kama matatizo tu ya kiakili.