Iceland kupiga marufuku tohara ya wanaume

Muswada huo unasema kuwa tohara hiyo hutekelezwa bila kutilia maanani uchungu unaompata mwathiriwa
Image caption Muswada huo unasema kuwa tohara hiyo hutekelezwa bila kutilia maanani uchungu unaompata mwathiriwa

Iceland iko katika harakati za kuwa taifa la kwanza barani Ulaya kupiga marufuku tohara ya wanaume huku kukiwa na ishara kwamba utamaduni huo unaotekelezwa sana na Wayahudi pamoja na Waislamu huenda ukazua hisia kali kuhusu uhuru wa kuabudu nchini humo.

Muswada ambao kwa sasa umewasilishwa mbele ya bunge la Iceland unapendekeza hadi miaka sita jela kwa mtu yeyote atakayetekeleza tohara hiyo isipokuwa tu kwa ajili ya sababu za kimatibabu.

Wakosoaji wanasema kuwa hatua hiyo ambayo imezua hisia miongoni mwa viongozi wa kidini barani Ulaya itafanya maisha ya Wayahudi na Waislamu nchini Iceland kuwa magumu.

Mmoja kati ya wanaume watatu dunia huwa amepashwa tohara sababu kuu ikiwa ya kidini au ile ya kitamaduni.

Wayahudi wengi na Waislamu wanahofia kwamba swala hilo linaweza kutumiwa kulenga dini hizo mbili wakitaja wasiwasi kama huo kuhusu mavazi ya kidini mbali na uchinjaji wa wanyama kwa lengo la kutumia nyama yao.

Muswada huo unasema kuwa tohara ya wavulana wadogo inakiuka haki yao ya kibinaadamu na ni kinyume na azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya mtoto.

Inaangazia swala hilo sambamba na lile la ukeketaji wa wanawake ambao tayari umepigwa marufuku katika mataifa kadhaa ya bara Ulaya.

Muswada huo unasema kuwa tohara hiyo hutekelezwa bila kutilia maanani uchungu unaompata mwathiriwa na kuongezea kuwa hatua hiyo hutekelezwa katika nyumba ambazo sio safi bila madaktari bali na viongozi wa dini.

''Kuna hatari kubwa ya maambukizi chini ya hali hiyo ambayo huenda ikasababisha kifo.mUswada huo unasema kuwa wazazi wana haki ya kutoa mwelekeo wa kidini kwa watoto wao, lakini haki hizo haziwezi kuwa juu ya haki za mtoto'', unasema muswada huo.

Wavulana wanaotaka kupashwa tohara kutokana na sababu za kidini au kitamaduni wanaweza kufanya hivyo watakapofikisha umri ambao wanaelewa ni nini kinachoendelea wakati wa tohara hiyo.

Taifa la Iceland lina takriban raia 336,000 ikiwemo jamii za Wayahudi na Waislamu.

Linadaiwa kuwa na Wayahudi 250 na Waislamu 1,500.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii