Mauaji ya mwanafunzi Tanzania: Polisi wawahoji maafisa wakuu wa Chadema

Marehemu Akwilina Akwiline Haki miliki ya picha PAUL WILLIAM SABUNI
Image caption Marehemu Akwilina Akwiline

Maafisa wa polisi mjini Dar es Salaam wamewataka viongozi wakuu wa chama cha upinzani nchini humo Chadema kufika mbele yake ili kuhojiwa kutokana na kifo cha mwanafunzi wa chuo kikuu cha usafirishaji nchini humo Akwilina Akwiline.

Bi Akwiline alifariki baada ya kupigwa risasi kimakosa wakati wa maandamano ya viongozi wa chama hicho yaliotibuliwa na maafisa wa polisi siku ya Ijumaa.

Mauaji hayo kwa sasa ndio swala linalozungumziwa sana nchini Tanzania huku raia kupitia mitandao tofauti ya kijamii wakishutumu kisa hicho.

Kulingana na gazeti la The Citizen nchini humo, taarifa kutoka kwa mkurugenzi wa itifaki ,mawasiliano na maswala ya kigeni John Mrema ilisema siku ya Jumatatu kwamba kiongozi wa uchunguzi wa eneo maalum la Dar es Salaam aliamrisha viongozi saba wa chama hicho kuripoti katika afisi yake ili kuhojiwa.

Orodha ya wale waliotakiwa kuripoti ni pamoja na mwenyekiti wa chadema Freeman Mbowe, katibu mkuu Vincent Mashinji na naibu katibu mkuu wa chama hicho wa Tanzania bara John Mnyika.

Wakati huohuo wakaazi wa mji wa Dar es salaam wataupungia mkono wa buriani mwili wa msichana huyo katika uwanja wa taasisi ya NIT siku ya Alhamisi kabla ya mazishi yake yanayotarajiwa kufanyika katika eneo la Rombo Kilimanjaro siku ya Ijumaa.

Image caption Jamaa ndugu na marafiki wakutana nyumbani kwa marehemu kuomboleza

Wakati huohuo ripoti ya upasuaji imesema kuwa bi Akwilina alifariki kutokana na shambulio la risasi katika kichwa chake.

Kulingana na gazetila The Citizen Tanzania Familia ya mwanafunzi huyo ilithibitisha kuwa ilipatiwa ripoti ya matokeo hayo iliofanywa katika hospitali ya Muhimbili.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa risasi hiyo iliingia kichwani kupitia upande wa kushoto na kutoka na upande wa kulia....'''alijeruhiwa vibaya'' , alisema nduguye marehemu bwana Festo Kavishe.

Aliongezea kuwa familia ilitosheka na ripoti hiyo na sasa inakamilisha maandalizi ya mazishi yake.

''Ningependa kusema kuwa tumetosheka na ripoti iliowasilishwa mbele yetu , kile tulichotaka ni picha kamili ya vile alivyouawa''.

Akwilina alifariki siku ya Ijumaa baada ya kupigwa risasi alipokuwa ndani ya daladala.

Image caption Akwilina alifariki siku ya Ijumaa baada ya kupigwa risasi alipokuwa ndani ya daladala.

Kulingana na ripoti za mapema ni kwamba maafisa wa polisi walikuwa wakijaribu kuwatawanya waandamanaji kwa kile walichokitaja kuwa maandamano haramu yaliofanywa na Chadema wakati ambapo risasi hiyo ilipita katika kioo cha nyuma cha daladala na kumpiga kichwa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii