Marubani wa Kenya kurejea baada ya kutekwa

Ndege ya marubani wa Kenya ilianguka na kusababisha kifo cha mtu mmoja na mifugo
Maelezo ya picha,

Ndege ya marubani wa Kenya ilianguka na kusababisha kifo cha mtu mmoja na mifugo

Waasi wa Sudani kusini wamewaachia marubani wawili wa Kenya waliotekwa zaidi ya mwezi mmoja uliopita baada ya ndege yao kupata ajali.

Msemaji wa waasi alisema wakenya hao waliachiwa baada ya kampuni ya bima kulipa zaidi ya dola za marekani 100,000 kulipa fidia ya kifo cha mtu mmoja aliyepoteza maisha baada ya ndege kuanguka.

Baada ya kutekwa kwa zaidi ya mwezi mmoja, Kepteni Pius Frank Njoroge na msaidizi wa rubani Kennedy Shamalla wameripotiwa kuwasili salama mjini Juba.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ameiambia BBC kuwa wawili hao watarejea Kenya baadae leo.

Waasi waliwashikilia watu hao ndege yao ilipoanguka katika mji wa Upper Nile na kuripotiwa kumuua mwanamke mmoja na mifugo.

Awali waasi walitaka zaidi ya dola 200,000 lakini walifikia makubaliano baada ya majadiliano na maafisa wa Kenya.

Msemaji wa waasi amesisitiza kuwa malipo hayo sio kikombozi bali ni fidia baada ya ajali hiyo kusababisha vifo.