Korea Kaskazini ilivyoufuta mkutano wa makamu wa rais wa Marekani Mike Pence

US Vice-President Mike Pence in front of North Korea's Kim Yong-nam (C) and Kim Yo-jong (R) Haki miliki ya picha Pool
Image caption Mike Pence aliketi mbele ya wajumbe wa Korea Kaskazini wakati wa sherehe za ufunguzi

Maafisa wa Marekani wanasema wajumbe wa Korea Kaskazini walijiondoa ghafla kutoka kwa mkutano wa faraghani uliokuwa umepangwa kufanyika mjini Seoul, Korea Kusini saa mbili kabla ya mkutano huo kufanyika.

Mkuu wa watumishi wa Pence, Nick Ayres, amesema makamu huyo wa Rais alikuwa amepangiwa kukutana na wajumbe wa Pyongyang akiwemo Kim Yo Jong - dadake kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un.

Mkutano huo ulipangiwa kuandaliwa siku ya sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya majira ya Baridi mapema mwezi huu.

Bw Pence alikuwa amezuru Seoul kuhudhuria

Lakini Bw Ayres amesema maafisa wa Korea Kaskazini waliufuta mkutano huo baada ya Pence kushutumu Korea Kaskazini kwa ukiukaji wa haki za kibinadamu na pia kutangaza mpango wa kuiwekea vikwazo zaidi vya kiuchumi.

Iwapo ungefanyika, basi ungekuwa mkutano wa kwanza rasmi kati ya Korea Kaskazini na maafisa wa utawala wa Rais Donald Trump ambaye amekuwa akiishutumu vikali Korea Kaskazini.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Heather Nauert alisema uwezekano wa kufanyika kwa mkutano mfupi kati ya wajumbe wa Korea Kaskazini na Bw Pence ulipotokea, makamu huyo wa rais alikuwa "tayari kutumia fursa hiyo kufikisha ujumbe kuhusu haja ya Korea Kaskazini kuacha mpango wake wa kustawisha makombora na silaha za nyuklia."

"Dakika za mwisho, Maafisa wa DPRK (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea) waliamua kutoendelea na mkutano huo. Tunasikitishwa sana na kukosa kwao kutumia fursa hii," alisema kwenye taarifa.

Hatua ya Korea Kaskazini kuamua kushiriki Michezo ya Olimpiki ya majira ya Baridi katika taifa hilo jirani ilikuwa imetazamwa na wengi kama ishara ya kuimarika kwa uhusiano katika rasi ya Korea.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kim Yo-jong, dada yake kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, akitazama mchezo na rais wa Korea Kusini Moon Jae-in

Lakini bado ulikuwepo wasiwasi kwamba Pyongyang, ambayo imekuwa ikishutumiwa vikali kwa kufanyia majaribio makombora ya masafa marefu na silaha za nyuklia, ilikuwa inatumia michezo hiyo kuimarisha sifa zake katika ngazi ya kimataifa.

Marekani - pamoja na nchi nyingine za Magharibi - imetahadharisha dhidi ya kupunguzwa kwa shinikizo dhidi ya Korea Kaskazini kuhusu hitaji la kusitisha mpango wake wa silaha za nyuklia pamoja na kuimarisha rekodi yake ya haki za kibinadamu.

Bw Ayers, amesema Korea Kaskazini ilikuwa imetumia "mkutano huo kama chambo kwa matumaini kwamba makamu huyo wa rais angelegeza msimamo wake, jambo ambalo lingewapatia fursa ya kujiimarisha kwa propaganda wakati wa michezo hiyo ya Olimpiki."

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Timu ya mpira wa magongo ya wanawake ya Korea ilijumuisha wachezaji kutoka Korea Kusini na Kaskazini

"Utawala wetu utasimama kidete dhidi ya haja ya Kim ya kuuhadaa ulimwengu kwa kuupamba utawala wake kwa picha za propaganda wakati wa Olimpiki. Pengine ndiyo sababu wakajiondoa kutoka kwa mkutano huo au pengine hawakuwa na nia njema kabisa hata walipokubali kushiriki mkutano huo," alisema.

Baada ya kuondoka Seoul, Bw Pence alisema Marekani na washirika wake hawatayumba katika msimamo wao dhidi ya Korea Kaskazini.

"Hakuna mabadiliko yoyote kati ya Marekani, Korea Kusini na Japan kuhusu haja ya kuendelea kuitenga Korea Kaskazini kiuchumi na kidiplomasia hadi wasitishe mpango wao wa nyuklia na makombora ya masafa marefu."

Hata hivyo, Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in amesema bado anatafakari uwezekano wake wa kukubali mwaliko wa Kim Jong-un na kuzuru Pyongyang.

Mkutano huo ukifanyika, basi itakuwa mara ya kwanza kwa viongozi wa mataifa hayo mawili kukutana katika kipindi cha zaidi ya mwongo mmoja.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii