Matumaini kwa msichana anayetokwa na machozi ya damu

Nikki Christou Haki miliki ya picha FERGUS WALSH/BBC

Watafiti wanasema wanasema wamegundua kasoro kwenye vinasaba ambayo wanaamini ndiyo husababisha ugonjwa kwenye mishipa ya damu ambao huwafanya wagonjwa kuvuja damu kwa njia ya kushangaza.

Ugonjwa huo pia husababisha kiharusi.

Ugunduzi wao unatoa matumaini kwa wasichana wawili ambao wamekuwa wakitokwa na damu machoni.

Wanasayansi katika Chuo Kikuu cha London katika Taasisi ya Afya ya Watoto na Hospitali ya Great Ormond Street (GOSH), ambao walishiriki utafiti huo, wamesema hiyo ni hatua kubwa katika kufahamu na kupata tiba ya ugonjwa huo wa kasoro kwenye mishinda ya damu ambao kwa kifupi hufahamika kama AVM.

Aidha, wanaamini kwamba baadhi ya dawa zinazotumiwa kutibu saratani zinaweza kutumiwa kutibu ugonjwa huo.

AVM, ugonjwa ambao huendelea kuwa mbaya zaidi kadiri mgonjwa anavyokua, husababisha kufura na pia ulemavu kwenye viungo.

AVM huhusisha kukusanyika kwa mishipa ya damu kwa wingi kuliko kawaida katika eneo ambalo mishipa mikubwa ya damu ya kusafirisha damu yenye oksijeni kwenye viungo mwilini huungana na mishipa miembamba ya kurejesha damu moyoni.

Wataalamu London, Edinburgh na Cambridge walishirikiana katika utafiti huo.

Walichunguza sampuli za viungo kutoka kwa watoto 160 ambao mishipa yao ilikuwa na kasoro mbalimbali zikiwemo AVM na kisha wakachunguza vinasaba (DNA) kwenye sampuli hizo.

Walipata jeni nne zenye kasoro ambazo zinaweza kusababisha tatizo hilo, zote ambazo huhusika katika mawasiliana kati ya sehemu ya juu ya seli na chembe cha ndani cha seli.

Kasoro hizo za jeni pia huhusika katika ueneaji wa aina nyingi za saratani.

Kuna dawa kadha ambazo hutumiwa kutibu kasoro za aina hiyo, na hii ina maana kwamba zinaweza pia kutumiwa kwa wagonjwa wenye tatizo hilo.

Dkt Veronica Kinsler kutoka GOHS aliyeongoza utafiti huo alisema: "Hii ni hatua kubwa sana kwetu."

Mmoja wa wagonjwa walioshirikishwa katika utafiti huo ni Nikki Christou, 13.

Ana tatizo la AVM upande wa kulia wa uso wake na kwenye fuvu la kichwa.

Anaweza kuvuja damu kwa wingi ghafla wakati wowote.

Image caption Msichana mwingine Marnie-Rae Harvey hutokwa na damu machoni lakini madaktari hawaelewi chanzo chake ni nini

Nikki anasema: "Inaweza kuogofya sana kwani damu hutoka kupitia pua na pia inaweza kutoka kupitia koo au mdomo. Wakati mwingine inaweza kuvuja kupitia mishipa yangu ya machozi na hivyo kunifanya nitokwe na damu badala ya maji.

"Ninaweza kujisikia kama napepesuka, na ninapovuja damu sana wakati mwingine huhitaji kubebwa kwa gari la kusafirisha wagonjwa hadi hospitalini."

Nikki amefanyiwa upasuaji mara 30 na hutembelea daktari mara kwa mara.

Nikki sasa ni mmoja wa wagonjwa wawili wanaopokea matibabu ambayo kawaida hutumiwa kutibu saratani kwa matumaini kwamba naye atapona.

Nikki amekuwa akimeza tembe moja kila siku kwa zaidi ya miezi sita.

Uchunguzi wa MRI wa karibuni umedokeza kwamba hali yake ya AVM haijakuwa mbaya zaidi, lakini itachukua zaidi ya mwaka mmoja kwa madaktari kufahamu iwapo tiba hiyo itafanikiwa.

Majaribio makubwa ya dawa hizo za saratani yanapangiwa baadaye.

Nikki ana ukurasa kwenye YouTube kwa jina Nikki Lilly ambapo hufuatiliwa na watu zaidi ya 300,000 na alishinda tuzo ya Junior Bake Off ya CBBC ya 2016.

Amewahi kumhoji pia waziri mkuu wa Uingereza.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii