Kabwe: Tutaendelea kupambana dhidi ya sheria kandamizi Tanzania

Zitto Kabwe,Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo
Maelezo ya picha,

Zitto Kabwe,Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Zitto Kabwe ameachiliwa huru kwa dhamana asubuhi hii baada ya kukamatwa na polisi usiku wa kuamkia Februari 23mkoani Morogoro, karibu kilomita 200 kutoka Dar es salaam.

Sababu ikitajwa ni kufanya mikutano bila kibali alipokuwa akifanya ziara ya kutembelea viongozi wa chama chao cha ACT Wazalendo maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Alipokamatwa Bw Zitto aliweka ujumbe katika akaunti yake ya Twitter, "Ninasindikizwa hadi kituo cha polisi cha Mgeta wilayani, Mvomero.... Sijaambiwa kwa nini nimekamatwa."

Mbunge Zitto Kabwe ameachiwa kwa dhamana ya maneno yenye thamani ya shilingi milioni 50 fedha za kitanzania na kudhaminiwa na wakaili wake ndugu Emmanuel Lazarus Mvula.

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo alikuwa kwenye ziara ya chama chake mkoani humo.

Ametakiwa kuripoti Polisi Kituo Kikuu cha Polisi cha Mkoa wa Morogoro Jumatatu, Machi12, 2018.

Baada ya kuachiwa kwa dhamana, Zitto Kabwe na viongozi wengine wa kitaifa wa chama hicho wamesema wataendelea na ziara ya kutembelea kata zinazoongozwa na chama hicho.

Vile vile Zitto akaelezea katika ukurasa wake wa Facebook " Baada ya kulala bure jana polisi Morogoro, tunaendelea na kazi yetu ya kutembelea kata zote ambazo Wananchi walitupa dhamana kwa kuchagua madiwani wa Act Wazalendo."

Katika eneo hilo hilo, taarifa za usiku wa kuamkia leo, zinasema mjumbe mwingine kutoka chama cha upinzani cha CHADEMA ameuwawa. Taarifa zinasema Diwani huyo wa kata ya Namwawala Godfrey Luena alikutwa nyumbani akiwa mauti baada ya kukatwakatwa kwa mapanga na watu wasiojulikana.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, Jeshi la polisi mkoani Morogoro limethibitisha tukio hilo na Kamanda wa mkoa humo Ulrich Matei amesema chanzo cha mauaji hayo huenda ikawa ni ulipizwaji wa kisasi kutokana na tukio la mauaji ya aina kama hiyo lililowahi kujitokeza miaka ya nyuma.