Mabadiliko ya wapenzi yaliyogusa nyoyo za wengi Kenya

Githae na Njeri Haki miliki ya picha Muchiri Frames

Kwa wengi, mwezi wa Februari ambao kawaida umekuwa ukihusishwa na mapenzi unakaribia kufikia ukingoni, na wengi wameanza kuisahau Siku ya Wapendanao.

Kwa Samuel Githae na Zipporah Njeri, siku hii maarufu kwa upendo ilikuwa mwanzo wa matukio ambayo yamechangia kuinuliwa kwao kutoka kwa maisha ya kutotambuliwa mjini hadi kuwa watu mashuhuri.

Wamekuwa bila makao rasmi, wakilala barabarani, kwenye vituo vya filamu na wakati mwingine katika nyumba za marafiki zao.

Lakini sasa watahamia katika nyumba mpya rasmi Jumamosi, ambayo wamelipiwa kodi na mhisani.

Isitoshe, wataabiri ndege kwa mara ya kwanza kwenda likizoni katika hoteli moja ya ufukweni pwani ya Kenya wiki ijayo.

"Siamini kwamba nitapanda ndege," Njeri aliambia BBC, akionekana mwenye furaha, akipigapiga mikono kama ndege anayejiandaa kupaa.

Yote yalianza kutokana na wazo la mpiga picha Johnson Muchiri kutoka kwa kampuni ya Muchiri Frames, na wafanyakazi wenzake, kutaka kufanya jambo la kipekee.

Huwezi kusikiliza tena
Mabadiliko ya wapenzi yaliyogusa nyoyo za wengi Kenya.

Jacinta Njoki alipojiunga na kampuni hiyo mwezi uliopita alitoa wazo la kuwashirikisha wapenzi ambao wanaishi mitaani.

Bi Njoki alikuwa amefanya kazi na watoto wa kurandaranda mitaani awali, akiwa na shirika alilolianzisha la Bin Beauty.

Alipolitoa wazo hilo, mara moja Bw Muchiri alilipokea na baadaye likaboreshwa na hatimaye mpango wa kuwatafuta wapenzi wa kupambwa zikaanza.

Bi Njoki alipotembea katika bustani ya Central Park jijini Nairobi kutana na kijana kwa jina Laban Njambi ambaye waliwahi kufahamiana awali akifanya kazi na shirika lake la Bin Beauty.

Alimwuliza iwapo alikuwa na mpenzi lakini akawa hana. Hata hivyo, alimfahamisha kuhusu rafiki yake, Samuel, ambaye alikuwa na mpenzi.

Haki miliki ya picha MUCHIRI FRAMES

Walimtafuta na akakubali kushiriki katika mpango huo lakini Njeri, ambaye mtaani hufahamika kama Virginia, alipofahamishwa kuhusu mpango huo, alikuwa na wasiwasi kidogo.

Alikuwa anahofia kwamba Bw Muchiri na wenzake wangekuwa kama wapiga picha wa awali ambao huwatumia watoto wanaorandaranda mitaani kujifaidi kisha kuwaacha wakiendelea kuteseka.

Hatimaye alikubali.

Picha zilipigwa katika kipindi cha siku mbili kabla ya Siku ya Valentine kwa sababu siku yenyewe maeneo mengi ambayo walipanga kupigiwa picha yangekuwa yamejaa watu.

Haki miliki ya picha MUCHIRI FRAMES
Image caption Bw Muchiri na mwenzake Bi Njoki

Siku ya kwanza walikuwa na mavazi yao ya kawaida na ya pili wakiwa na mavazi mapya katika Makumbusho ya Shirika la Reli.

Baadaye jioni, walipelekwa katika hoteli moja ya kifahari kwa chakula cha jioni mtaa wa Westlands kwa gharama ya rafiki mwingine wa Bw Muchiri ambaye pia alijitolea.

Kisa chao ambacho kimesimuliwa kupitia picha kiliwasisimua Wakenya sana katika mitandao ya kijamii wengi wakifurahia mabadiliko ambayo yalitokea kwa wawili hao.

Haki miliki ya picha MUCHIRI FRAMES

Wengi walijitolea kuwasaidia Samuel na Zipporah, wote ambao umri wao ni miaka 20.

Picha za kabla yao kupambwa na kubadilishwa mavazi na za baada yao kupambwa na kuvalia nguo na viatu vipya pamoja na Njeri kusukwa nywele, Githae naye akanyolewa nywele zake kwa mtindo wa kisasa zinaonesha mabadiliko hayo.

Mwanzoni, wanaonekana kama vijana wa kawaida wa kurandaranda mtaani lakini kwenye picha za baadaye wanaonekana kutabasamu na kujawa na matumaini tele.

Ukazitazama picha za baadaye bila kuziangazia sana, unaweza kudhania wawili hao ni wanamitindo au wapenzi kutoka familia tajiri.

Githae mwenyewe ameambia BBC kwamba muonekano mpya wa mpenzi wake ulimshangaza.

"Sijawahi kumuona akiwa mweupe hivyo, akiwa maridadi," amesema.

"Mimi nilikuwa naonekana kijana, zamani alikuwa anasema nimezeeka."

Haki miliki ya picha MUCHIRI FRAMES

"Kubadilishwa kwao na kuonekana kama wanamitindo pengine ndio mfano halisi zaidi wa mtu kupata fursa ya pili maishani," aliandika Saddique Shaban kwenye Twitter.

Njeri Mwangi, akimjibu Shaban aliandika: "Bila shaka. Unajipata ukitaka kutazama mabadiliko hayo tena na tena! Inapendeza sana."

"Hadithi yao ya mapenzi inagusa moyo sana na ni ya kutia moyo," kampuni ya safari za kitalii ya Bonfire Adventures and Events imeandika kwenye ukurasa wake wa Facebook, ikitangaza pia kujitolea kwao kuwalipia wawili hao likizo katika hoteli ya kifahari ufukweni eneo la Diani.

Bw Muchiri ataandamana na wapenzi hao kunakili "hadithi yao wakifurahia ufukweni".

Kampuni hiyo pia imeahidi kuwalipia kodi kwa miezi mitano.

Githae na Njeri wote wawili wanasema mabadiliko ambayo yalitokea kwao ni ishara kwamba vijana na watoto wa mitaani ni watu wa kawaida.

Wana mapenzi ya dhati yanayodumu.

Wote wawili wanatafuta kazi ambayo wanaamini itawasaidia kudumisha maisha yao ya sasa baada yao kuondolewa barabarani.

Njeri, ambaye alifika Nairobi miaka miwili iliyopita baada ya kuahidiwa nafasi ya kazi na rafiki yake lakini akajipata akilala barabarani, angependa kufanya kazi katika hoteli.

Githae ni dereva aliyehitimu na ana leseni, baada ya kupokea mafunzo kupitia udhamini wa mhisani.

Akipata pesa, aliambia BBC kuwa anapanga kuwasaidia ndugu zake ambao pia wanateseka.

Wanaishi na jamaa zao baada ya mama yao kufariki.

Njeri hajawahi kurejea kwao nyumbani na jamaa zake bado wanaamini anafanya kazi, lakini sasa baada ya hali yake kubadilisha angependa kuwatembelea na kuwajulia hali.

Muchiri anasema mapambo na mabadiliko waliyowafanyia wawili hao yote yaligharimu takriban $450, ingawa binafsi alitumia takriban $200 hivi.

Marafiki zake walijitolea kwa nguo, kumpodoa Njeri, na mengine mengi.

Njeri anasema watu wa kawaida hawafai kuwadharau watu wanaoteseka au kupitia dhiki.

"Pesa ndizo chanzo cha maovu," anasema, huku akinukuu Biblia.

Mada zinazohusiana